Trier kuadhimisha miaka 200 ya kuzaliwa Karl Marx
5 Mei 2018"Tuna matumaini kwamba kila mmoja ambaye atataka kushughulika na suala hili la Marx atafanya hivyo katika njia ya utulivu," msemaji wa mji huo Michael Schmitz alisema. "Iwapo unataka kumkosoa Marx , unakaribishwa kufanya hivyo, lakini sio kwa kutumia nguvu na ghasia ama hasira za uharibifu."
Sherehe ya ufunguzi Ijumaa jioni mjini Trier ilianza kwa hotuba iliyotolewa na rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker.
"Unapaswa kumuelewa Karl Marx katika wakati wake," Juncker alisema, na kuongeza kwamba Marx hawezi kuwajibishwa kutokana na uhalifu uliotendwa na wafuasi wake muda mrefu baada ya kifo chake mwaka 1883.
Maonesho makubwa matatu yanatarajiwa kufunguliwa kwa ajili ya umma kuanzia leo Jumamosi.
Lakini kilele cha sherehe hizo za siku ya kuzaliwa kinatarajiwa kuwa leo Jumamosi , wakati picha kubwa ya Marx , iliyotolewa zawadi na China , inatarajiwa kuzinduliwa. Makamu mkuu wa chama cha waandishi cha PEN nchini Ujerumani kimeomba kwamba uzinduzi ucheleweshwe, hata hivyo, hadi pale mshairi kutoka China Liu Xia atakapoachiliwa kutoka kizuwizi cha nyumbani na kuondoka nchini China.
Wakosoaji na waandamanaji wanatarajiwa kuonekana na kueleza kile wanachosimamia. Chama kinachopinga wahamiaji cha Alternative for Germany AfD kinapanga kumbukumbu ya wahanga wa ukomunisti kwa maandamano ya kimya kimya, na ukeshaji sehemu kadhaa kwa ajili ya kupigwa marufuku kwa vuguvugu la kidini nchini China la Falun Gong pia yanapangwa kufanyika.
Maandamano ya waungaji mkono nadharia za Marx
Wakati huo huo , muungano wa waungaji mkono nadharia ya Marx , ikiwa ni pamoja na wanachama wa chama cha Die Linke , chama cha mrengo wa kushoto nchini Ujerumani pamoja na chama cha Kikomunist nchini Ujerumani, pia vimepanga kufanya maandamano "dhidi ya ubepari na unyonyaji."
Kwa mujibu wa polisi maandamano ya upande mwingine dhidi ya yale ya chama cha AfD pia yanapangwa kufanyika. Polisi watakuwapo pamoja na maafisa kadhaa wa mjini Trier. "Idadi kubwa ya mikutano na matukio yanaleta changamoto ya aina yake," mkuu wa polisi Ralf Kraemer amesema.
Katikati ya mji wa Trier , katika jimbo la Rhineland-Palatinate kumewekwa maandishi maalum "Karl Marx (1818-1883), Maisha - Kazi - Ushawishi hadi sasa" - ambako zaidi ya maonesho 400 kutoka karibu dazeni moja ya majimbo nchini Ujerumani katika makumbusho mbili za mjini Trier yatafanyika.
Pia kuna maonesho mawili ya washirika katika makumbusho ya mji huo ya Kanisa na katika nyumba ya Karl Marx , sehemu alipozaliwa.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae
Mhariri: Caro Robi