1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TRIPOLI:Libya yaadhimisha siku ya mapambano dhidi ya Wataliano kwa kufunga laini za simu.

27 Oktoba 2005
https://p.dw.com/p/CEO1

Serikali ya Libya leo imekata njia zote za mawasiliano ya simu kuingia nchini humo kutoka nje wakiwa wanaadhimisha siku inayoitwa siku ya mapambano,wakikumbuka na kupinga uhalifu uliofanywa na Wataliani,wakati walipokuwa wakiikalia nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika,katika kipindi cha nusu ya kwanza ya karne ya 20.

Ujumbe wa simu unaotolewa kwa lugha ya Kiarabu na Kiingerea,unawafahamisha watu wanaopiga simu namba za Libya wakitokea nje ya nchi hiyo,kuwa mawasiliano ya kimataifa yamezuiliwa hadi itakapofika saa 12 jioni ya leo,nchi hiyo ikiwa katika kumbukumbu ya madhila ya uhalifu waliyotendewa na Wataliani.

Libya ilikuwa chini ya himaya ya jeshi la Italia kati ya mwaka 1911 hadi mwaka 1912 kabla haijawa kuloni la Italia katika miaka ya 1930.

Libya inadai kutoka Italia fidia ya madhila waliyotendewa kwa kujengewa barabara kubwa itakayogharimu euro bilioni sita,gharama ambazo kwa sasa ni kubwa mno kwa serikali ya Italia kulipa.

Wakati wa mkutano baina ya Waziri Mkuu wa Italia Silvio Berlusconi mjini Tripoli mwezi kama huu mwaka jana,rais wa Libya Moamer Gadafi alikubali jina la siku ya leo libadilishwe kutoka siku ya kulipiza kisasi na kuwa siku ya urafiki na watu wa Italia.

Hata hivyo kwa mujibu wa Libya,italia haijatimiza ahadi hiyo iliyoiweka mwaka jana.