1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aahidi mkataba mnono wa kibiashara na Uingereza

4 Juni 2019

Rais wa Marekani Donald Trump ameiahidi Uingereza mkataba mnono wa kibiashara baada ya nchi hiyo kujiondoa katika Umoja wa Ulaya, na akaapa kuondoa tofauti zozote zilizopo kati yake na Uingereza kuhusu suala la Huawei

https://p.dw.com/p/3Jpmw
Großbritannien US-Präsident Donald Trump & Theresa May, Premierministerin
Picha: Reuters/S. Rousseau

Rais wa Marekani Donald Trump ameiahidi Uingereza mkataba mnono wa kibiashara baada ya nchi hiyo kujiondoa katika Umoja wa Ulaya, na akaapa kuondoa tofauti zozote zilizopo kati yake na Uingereza kuhusu jukumu la kampuni ya China ya Huawei kutengeneza mitandao ya 5G. 

Baada ya kukaribishwa kwa heshima na Malkia Elizabeth II katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kiserikali nchini Uingereza, Trump aligeukia siasa leo na kumpongeza Waziri Mkuu anayeondoka Theresa May na akawataja viongozi wawili aliosema wana sifa za kuweza mumtrithi May.

Proteste gegen Donald Trump in London
Waandamanaji walijitokeza London kumpinga Trump Picha: Reuters/C. Kilcoyne

Kuanguka kwa uwaziri mkuu wa May kuhusu mpango wa Brexit kulizusha wasiwasi kuwa Trumpo angemuaibisha hadharani. Badala yake, Trump aliweka pembeni maneno matupu ambayo yangemfedhehesha na akamsifia kwa kuyataja hata maswala ambayo ni nyetu kabisa kama vile Huawei na anayefaa kumrithi

Trump alimtaja Boris Johnson, ambaye amesema Uingereza inapaswa kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya Oktoba 31, iwapo itakuwa imefikia makubaliano au la na Jeremy Hunt, waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Uingereza ambaye anaonya dhidi ya kuondoka bila makubaliano.

Alipoulizwa kama uamuzi wa muda wa mawaziri wa Uingereza kuiruhusu Huawei kuwa na jukumu dogo  katika mitandao ya simu ya 5G unaweza kuathiri ushirikiano wa masuala ya usalama na mshirika mkuu wa Uingereza, Trump alisema atayashughulikia maswala hayo.

Kuhusu Brexit, Trump alisema talaka ya Uingereza Umoja wa Ulaya itakamilika kwa kuwa Ungereza ni nchi nzuri sana inayotaka utambulisho wake, na udhibiti wa mipaka yake na inayotaka kuyaendesha masuala yake yenyewe. Na wakati nchi hiyo ikijiandaa kuondoka Ulaya, Marekani imedhamiria kufikia makubaliano mazuri kabisa kati ya nchi hizo mbili.

Rais huyo wa Marekani amesema amekataa kukutana na kiongozi wa upinzani wa Chama cha Labour Jeremy Corbyn, msoshalisti mkongwe ambaye alimkosoa Trump katika maandamano yaliyoandaliwa leo mjini London.