Trump ahoji umakini wa UN
27 Desemba 2016Rais huyo mteule wa Marekani ameandika kupitia ukurasa wake wa Twitter kwamba ingawa Umoja wa Mataifa ni taasisi yenye umuhimu mkubwa, lakini imekuwa kama kijiwe cha watu kukutana pamoja, kuzungumza na kufurahia maisha, akiongeza kuwa hiyo ni hali inayosikitisha.
Siku ya Ijumaa, Trump alionya kuyabadilisha maamuzi hayo yaliyolaaniwa vikali na Israel pindi akiingia madarakani hapo tarehe 20 mwezi ujao. Awali Wazizi Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alinukuliwa akisema wao na Marekani walikubaliana kutoliwasilisha suala hilo kwenye Umoja wa Mataifa kwa kuwa lingeweza kuhujumu juhudi za kusaka amani.
Alisema "Kwa miongo mingi, serikali za Marekani na Israel zimetofautiana kuhusu makaazi hayo, lakini tulikubaliana kuwa baraza la Usalama sio mahala pa kutatua suala hilo. Tulijua kuwa mazunguzmo yangekuwa magumu katika Baraza la Usalama na kuhujumu juhudi za amani. Nilimwambia John Kerry kuwa marafiki hawawapeleki wenzao katika Baraza la Usalama"
Kwa miongo kadhaa, Marekani imepinga ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Israel katika ardhi ambayo iliikamata wakati ya vita vya va Ashariki ya Kati vya mwaka 1967, ingawa haijawahi kuruhusu kura ya kupitisha azimio dhidi ya Israel. Viongozi wa nchi hizo mbili kwa muda mrefu wamekuwa wakitaka kufikiwa kwa makubaliano yatakayohusisdha kuwepo kwa taifa la Palestina, ambayo Netanyahu alieleza kukubaliana nayo.
Uamuzi uliochukuliwa na serikali ya Rais Barack Obama wa kutopiga kura ya azimio hilo kulaani makazi ya kilowezi ya Israel Ijumaa iliyopita, umeweka pembeni madai ya Trump kwamba Marekani ingelitumia kura yake ya turufu kuzuia, kama alivyokuwa amemuahidi Netanyahu hapo awali. Uamuzi huu pia umeashiria kilele cha mahusiano hasi yaliyodumu kwa miaka kadhaa kati ya utawala wa Rais Obama na Netanyahu, ambao kamwe hawakuwahi kupatana kwenye utatuzi wa mzozo wa Mashariki ya Kati.
Mnamo mwezi Disemba mwaka jana, Trump aliliambia shirika la habari la Associated Press kwamba asingetaka kuegemea upande wowote kuhusiana na masuala yahusuyo mzozo kati ya Israel na Palestina, lakini matamshi yake baada ya kuanza kampeni yalichukuliwa kama yanayounga mkono zaidi Waisrael, huku akitoa kauli za kashfa dhidi ya Wapalestina.
Ujumbe wake wa jana wa Twitter kuhusu Umoja wa Mataifa umepuuzia kazi kubwa iliyofanywa na nchi 193 wanachama wa Umoja huo, ambazo ni pamoja na kupitisha zaidi ya maazimio 70 ya kisheria, vikwazo vipya dhidi ya Korea Kaskazini, hatua za kukabiliana na mizozo na kuruhusu vikosi vya kulinda amani duniani, kulaani uvunjifu wa haki za binaadamu nchini Iran na Korea Kaskazini na kuruhusu uchunguzi wa uhalifu wa kivita nchini Syria.
Katika hatua nyingine, rais huyo mteule wa Marekani amemteua David Friedman kuwa balozi wa Marekani nchini Israel. Friedman anasifika kwa misimamo yake ya kukubaliana na ujenzi huo wa makazi ya kilowezi ya Israel, na anatajwa kuwa sehemu ya mpango wa Trump wa kugeuza mikakati ya Obama dhidi ya Israel. Hatua hiyo imezua mjadala mzito wakati ambapo kumeibuka wasiwasi mkubwa kati ya Marekani na Israel.
Mwandishi: Lilian Mtono/AP
Mhariri: Mohammed Khelef