1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aichanganya Ulaya kwa wito kuhusu wapiganaji wa IS

18 Februari 2019

Matakwa ya rais wa Marekani Donald Trump kwamba mataifa ya Ulaya yawachukuwe raia wake wanaopigana nchini Syria yamezusha sintofahamu, huku mataifa yakielezea wasiwasi kuhusu namna ya kuwashtaki magaidi hao wa IS.

https://p.dw.com/p/3Db78
Belgien Brüssel Treffen der EU-Außenminister | Heiko Maas
Picha: picture-alliance/AP/F. Seco

Swali la wapiganaji kama hao wa kigeni limekuwa kitendawili kwa mataifa ya Ulaya kwa miaka kadhaa. Wafungwa wa kundi hilo la Dola la Kiislamu wanakabiliwa na mateso au adhabu ya kifo iwapo watasalia kwenye magereza nchini Syria au Iraq, na Umoja wa Ulaya unapinga adhabu ya kifo.

Lakini ni mataifa machache ya Ulaya yalio na uwakilishi wa kibalozi nchini Syria au Iraq, achilia mbali mikataba ya urudishwaji wa watuhumiwa ambao ni raia wa mataifa hayo.

Kuthibitisha utambulisho wa nani ni nani na kukusanya ushahidi imara dhidi ya watuhumiwa watakaosimama katika mahakama za Ulaya ni suala lisilowezekana kimsingi.

Na pia kuna swali la nini cha kufanya juu ya wanawake na watoto wa wapiganaji wa Dola la Kiislamu.

Kisa cha msichana wa Kiingereza alietoroka na kwenda kujiunga na Dola la Kiislamu, ambaye amejifungua mtoto wa kiume na sasa anataka kurejea nchini Uingereza, kimeanzisha mjadala nchini humo kuhusu namna ya kushughulikia raia wanaojaribu kuondoka Syria mnamo wakati kundi hilo la kigaidi linasambaratika.

"Bila shaka siyo rahisi kama wanavyofikiria nchini Marekani," waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani heiko Maas aliwambia waandishi habari siku ya Jumatatu wakati wa mkutano wa mamwaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya.

Großbritannien Syrien Schülmädchen auf dem Weg nach Syrien SCHLECHTE QUALITÄT
Picha hii ya Februari 21, 2015 inawaonyesha mabinti wa Kiingereza (kushoto-kulia), Kadiza Sultana, Shamima Begum na Amira Abase waliotoroka na kwenda kujiunga na IS nchini Syria. Sasa Begum anataka kurudi nyumbani baada ya kujifungua mtoto wa kiume.Picha: picture-alliance/dpa/EPA/LONDON METROPLITAN POLICE

"Raia wa Ujerumani wana haki ya kurudi, lakini tuna uwezo mdogo nchini Syria kwa sasa kuhakiki iwapo raia wa Ujerumani kweli wameathirika."

Maas alisema mamlaka zitalaazimika "kuhakiki ni kwa kiasi gani walihusika katika mapigano kwa ajili ya IS, hatua ambayo itapelekea kufunguliwa mashtaka ya jinai dhidi yao."

"Watu hawa wanaweza tu kuja Ujerumani ikiwa imethibitishwa kuwa wanawaze kueplekwa rumande mara moja," alisema.

Hatari ya kiusalama

Wataalamu wa usalama wameonya kuwa magaidi waliotiwa hatiani wataachiwa huru kutoka magareza ya Ulaya kwa wingi katika kipindi cha miaka miwili ijayo, wengi wao wakiwa wamepata mafunzo na kupigana nchini Syria na Iraq, lakini hawakufunguliwa mashtaka mazito kutokana na kukosekana kwa ushahidi.

Wapiganaji wa Kifaransa ndiyo wengi zaidi kutoka taifa la Ulaya. Maafisa wa Ufaransa wana wasiwasi kwa sababu mwaka 2015 na 2016, kundi la Dola la Kiislamu la wapiganaji wa Ufaransa Ubelgiji lilivuka kutoka Syria na kuingia Uturuki, na hatimaye kufanya mashambulizi mabaya mjini Paris na Brussels.

"Ngome za mwisho za Daesh zinaanguka, na hali halimaanishi kuwa matendo ya Daesh yamemalizika. Ni kinyume chake," alisema waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian.

Uingereza inakataa kuwachukuwa raia wake waliojiunga na IS na imewavua uraia wao. Ubelgiji imesema huko nyuma kwamba haitafanya juhudi zozote kubwa kuwanusuru raia wake 12 waliofungwa nchini Syria na wawili walioko Iraq.

Mataifa mengine ya Ulaya yamesalia kimya kwa kiasi kikubwa kuhusu hatma ya wanaume na wanawake ambao wanawaona kama kitisho kwa usalama.

Syrien Frau und Kind eines vermeintlichen IS Kämpfers in Rakka
Mke wa mshukiwa wa kundi la IS akimbeba mwanae wakati akisubiri kuhojiwa mjini Raqa.Picha: Getty Images/AFP/B. Kilic

Waziri wa mambo ya nje ya Hungary Peter Szijjarto alisema suala hilo ni mojawapo ya "changamoto kubwa zaidi zinazotukabili katika miezi ijayo."

"Juhudi zetu kubwa sasa zinapaswa kuwa kutowaruhusu kurudi Ulaya," alisema Szijjarto, ambaye serikali yake yenye msimamo mkali dhidi ya uhamiaji imehusisha mashambulizi ya wafuasi wa itikadi kali na uhamiaji.

Lakini waziri wa mambo ya nje wa Slovakia Miroslav Lajcak, pia kutoka serikali inayopinga uhamiaji, alisema "bila shaka nitakubaliana na Ulaya kuwarejesha wapiganaji wa kigeni.

"Kuna haja ya kuainisha msimamo wa Ulaya kuhusu suala hili," Lajcak aliwaambia waandishi habari.#

"Tuupende au tusipende msimamo wa Marekani, hawafanyi siri kuhusu msimamo huo. Ni wazi kabisaa," alisema. "Huu ndiyo ushirika muhimu wa Umoja wa Ulaya. Lakini kanunu za ushirika huu zimebadilika na tunahitaji kuweza kuitikia hilo."

Seneta wa Marekani Bob Menendez wa chama cha Demokratic, akiwa ziarani mjini Brussels, alisema mataifa ya Ulaya yanapaswa kutafuta njia ya kushughulikia changamoto hiyo.

"Kama tuna mtu ambaye tumembaini vizuri chini ya sheria kama mtu ambaye ni mpiganaji wa ISIS basi tunapaswa kuwa na uwezo wa kuwashtaki iwe nyumbani au ugenini," alisema katika shirila la ushauri la Ujerumani la Wakfu wa Marshall.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape,dpae

Mhariri: Daniel Gakuba