1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aiondoa Marekani kwenye Mkataba wa Paris wa 2015

21 Januari 2025

Rais wa Marekani Donald Trump amesaini maagizo kadhaa ya rais yenye utata baada ya kuapishwa kama rais wa 47 wa nchi hiyo hapo Jumatatu.

https://p.dw.com/p/4pP0f
Rais wa Marekani Donald Trump akisaini maagizo ya rais
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: JIM WATSON/AFP

Miongoni mwa maagizo hayo ya rais aliyoyatia saini ni kuiondoa Marekani kutoka kwenye mkataba wa mazingira wa Paris wa mwaka 2015,kuwaachia huru walioyavamia majengo ya bunge mwaka 2021 na kujaribu kuzuia kuidhinisha kushindwa kwake na Joe Biden.

"Natumai wataachiwa huru leo kwa kweli," alisema Trump baada ya kusaini agizo hilo la msamaha.

Trump vile vile amesaini agizo la kuiondoa Marekani kutoka kwenye Shirika la Afya Duniani WHO na ametishia kuwawekea majirani zake Canada na Mexico ushuru mkubwa katika bidhaa zao.

Mtoaji mkubwa wa gesi chafuzi duniani

Na kwa kuiondoa Marekani kutoka kwenye mkataba wa mazingira wa Paris, Trump ameiondoa nchi ambayo ndiyo mtoaji mkubwa wa gesi chafuzi duniani, kutoka kwenye juhudi za ulimwengu za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kwa mara ya pili katika kipindi cha mwongo mmoja.

Rais Trump akionyesha agizo la rais alilolitia saini
Rais Trump akionyesha agizo la rais alilolitia sainiPicha: Mike Segar/REUTERS

Trump ametia saini amri hiyo ya kuiondoa Marekani kwenye mkataba huo mbele ya wafuasi wake waliokuwa wamekusanyika katika uwanja wa Capital One Arena mjini Washington.

"Unafikiri Biden angeweza kufanya hivi? Sidhani," Trump aliwaambia wafuasi wake waliokuwa wakimshangilia huku akiwarushia kalamu alizotumia kusaini maagizo ya rais ya awamu ya kwanza.

Hatua hiyo inaiweka Marekani pamoja na Iran, Libya na Yemen kama nchi za pekee duniani ambazo haziko kwenye mkataba huo wa Paris wa mwaka 2015.

Uchimbaji mafuta kuanza tena Marekani

Katika hotuba yake baada ya kula kiapo, Trump alisema kwamba Marekani itaanza tena uchimbaji wa mafuta na gesi baada ya hatua hiyo kusitishwa na rais aliyeondoka mamlakani Joe Biden.

Uchimbaji wa gesi baharini
Uchimbaji wa gesi bahariniPicha: Albatross/Getty Images

Trump ambaye ni rais wa 47 wa Marekani amekuwa akipinga mabadiliko ya tabia nchi na kudai ni hekaya tu. Aliiondoa Marekani kutoka kwenye mkataba wa Paris alipoingia madarakani kwa mara ya kwanza, ingawa mchakato huo ulichukua miaka lakini Biden alisaini mara moja amri ya kuirejesha Marekani alipochukua uongozi.

Rais huyo mpya wa Marekani pia amesaini agizo la kutangaza dharura ya kitaifa katika mpaka wa Marekani na Mexico na kusema atapeleka kikosi cha majeshi kukabiliana na uhamiaji haramu - suala muhimu wakati wa kampeni lililompelekea kupata ushindi dhidi ya Kamala Harris.