Trump akaribia uteuzi wa chama chake huko New Hampshire
22 Januari 2024Hii ni baada ya gavana wa Florida Ron DeSantis kujiondoa chini ya saa 48 kabla ya mchujo wa New Hampshire kesho Jumanne.
Kwa mtizamo wa hali ilivyo, ratiba ya uteuzi wa Trump kuwa mgombea wa Republican atakayekabiliana na Rais Joe Biden katika uchaguzi wa Novemba mwaka huu, inaweza kutimia mapema sana, kwani kuna nafasi ndogo kwake kushindwa na mshindani pekee aliyesalia dhidi yake Nikki Haley katika jimbo la New Hampshire.
DeSantis aliyetazamwa na Republican kama mbadala wa Trump kuelekea uchaguzi mkuu mwezi Novemba, alitangaza kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho jana Jumapili na kusema atamuunga mkono Donald Trump.
Biden aonya juu ya urais wa Donald Trump wakati wa kukumbuka uvamizi wa jengo la Bunge
"Lakini siwezi kuwaomba wafuasi wetu wajitolee wakati wao na kuchangia rasilimali zao. Hatuna njia wazi ya ushindi. Kwa hiyo, leo nasimamisha kampeni yangu. Ninajivunia kutimiza 100% ya ahadi zangu na sitaacha sasa. Ni wazi kwangu kwamba wapiga kura wengi wa mchujo wa chama cha Republican wanataka kumpa Donald Trump nafasi nyingine," amesema DeSantis.
Wiki iliyopita, rais huyo wa zamani Donald Trump alipata ushindi mkubwa dhidi ya DeSantis katika jimbo la Iowa, huku Haley akishika nafasi ya tatu. Ikumbukwe kuwa hakuna mgombea yeyote aliyewahi kushindwa kutwaa taji la Republican baada ya kutwaa majimbo mawili ya ufunguzi. Trump aanza vyema safari yake ya kuwania urais Marekani
Wapiga kura wenye misimamo huru wa New Hampshire
Hali hiyo inafanya kinyang'anyiro cha New Hampshire kuwa cha ushindani mkali hasa kwa Haley, ambaye anamfuata bosi wake wa zamani kutafuta tiketi ya Republican kwa kile kinachoonekana kama jimbo lake ambako ana wafuasi wengi zaidi. Haley aliwahi kuwa balozi wa Trump katika Umoja wa Mataifa.
Trump aongoza kinyang'anyiro cha kuwania urais
Wiki iliyopita, Trump mwenye umri wa miaka 77, alizidisha mashambulizi dhidi ya Haley, akisema "hana akili ya kutosha" na kudai kuwa hakupata heshima ya wapiga kura.
Jana Jumapili, alimshambulia tena huku akimsifu DeSantis kama "mtu mwenye uwezo mkubwa” alipokubali ridhaa ya gavana huyo mbele ya wafuasi wake waliokuwa wakimshangilia.
Kura za Maoni zamweka Nikki Halley nyuma ya Trump
Huku DeSantis akiwa amejiondoa kwenye kinyang'anyiro, Haley analenga kutegemea idadi kubwa ya watu wenye misimamo huru wa New Hampshire -- ambao wanaruhusiwa kupiga kura katika mchujo wa kila chama, na kwa kawaida huegemea zaidi upande wa wagombea wenye misimamo ya wastani. Baadhi ya wachambuzi wametaja kuwa jimbo la New Hampshire litakuwa nafasi yake ya mwisho.
Lakini wachambuzi wanasema itakuwa kazi ya kupanda mlima kwa Halley kwani yuko nyuma ya Trump kwa pointi 15 kwa mujibu wa kura za maoni zilizofanywa na mashirika ya RealClearPolitics na FiveThirtyEight. Isitoshe hivi karibuni, kasi ya kampeni zake imeonekana kupungua.
Iwapo Haley atafanya vyema siku ya Jumanne, hiyo inaweza kumfanya apate tena nguvu ya kampeni na kuonekana kama tishio la kweli kwa rais huyo wa zamani anayeelekea katika jimbo lake la South Carolina mwishoni mwa Februari.
Chanzo: AFPE