Trump akataa kutia saini tamko la pamoja mkutano wa G7
10 Juni 2018Rais Trump wa Marekani alimshambulia kwa kumtusi vibaya mwenyeji wa mkutano huo waziri mkuu wa Canada justin Trudeau.
Dakika chache baada ya taarifa ya pamoja ambayo iliidhinishwa na viongozi wa kundi la washirika saba kuchapishwa katika mji wa Canada wa Quebec ambao ulikuwa mwenyeji wa mkutano huo, Trump alianzisha mashambulizi katika ukurasa wa Twitter kutoka nje ya nchi hiyo akiwa katika ndege ya rais wa Marekani ya Air Force One.
Kiongozi huyo wa Marekani aliondoka mapema kutoka katika mkutano huo akiwa njiani kwenda Singapore katika mkutano wa kihistoria wa kinyuklia pamoja na kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un , na kuchukua hatua ya kutofautiana na matamshi ya waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau katika mkutano na waandishi habari kabla ya kuondoka nchini Canada.
"Kwa msingi wa matamshi yasiyo sahihi ya Justin katika mkutano na waandishi habari , pamoja na ukweli kwamba Canada inatoza ushuru mkubwa kwa wakulima wetu , wafanyakazi na makampuni nchini Marekani, nimewaagiza wawakilishi wetu wa Marekani kutoidhinisha tamko hilo la pamoja kwa kuwa tunaangalia kuhusu ushuru katika magari ukisababisha kufurika kwa magari ya katika soko la Marekani!. Trump aliandika katika ukurasa wa Twitter.
"Waziri mkuu Justin Trudeau wa Canada ameonekana kuwa msikivu na mtulivu wakati tulipokutana katika mkutano wa G7 lakini alibadilika na kutoa matamshi katika mkutano na waandishi habari baada ya mimi kuondoka kwamba .. hatakubali kuburuzwa.' ni uongo na dhaifu."
Wacaanda ni wapole lakini hawataburuzwa
Hapo mapema Trudeau aliwaambia waandishi habari kwamba uamuzi wa Trump kuweka usalama wa taifa kuhalalisha ushuru wa Marekani dhidi ya bidhaa zinazoingizwa nchini humo za chuma cha pua na bati , "ni aina ya tusi" kwa wanajeshi wa zamani wa Canada ambao walisimama pamoja na washirika wao wa Marekani katika mizozo ambayo ni pamoja na vita vikuu vya kwanza vya dunia.
"Wacanada ni wapole na waelewa lakini pia hatutakubali kuburuzwa," alisema.
Na alisema amemwambia Trump "itakuwa kwa masikitiko makubwa lakini itakuwa kwa uwazi kabisa na uthabiti kwamba tunasonga mbele na hatua za kulipiza kisasi ifikapo Julai mosi, kwa kuweka ushuru sawa na ule ambao Wamarekani wamehalalisha kwa kutuwekea."
Baada ya maandishi ya hasira ya Trump katika ukurasa wa Twitter , ofisi ya waziri mkuu Trudeau ilitoa jibu fupi: "tunalenga katika kila kitu tulichokamilisha hapa katika mkutano wa G7. Waziri mkuu hakusema kitu ambacho hajasema kabla , katika mazungumzo ya wazi na faragha na rais Trump.
Matamshi ya hasira
Matamshi ya hasira dhidi ya Trudeau , na pamoja na kundi la wanachama wengine wa G7, ni tukio lingine la hivi karibuni ambamo Trump amepambana na washirika wa karibu wa Marekani, hata wakati akiwa ametoa matamshi wa kutia moyo kwa viongozi wa kidikteta akma Kim na Vladimir Putin wa Urusi.
Wakati huo huo, ahadi ya karibu dola bilioni 3 kusaidia wanawake walioko katika hali duni na wasichana, ikiwa ni pamoja na wakimbizi kupata elimu ilitangazwa katika mkutano wa kilele wa G7 siku ya Jumamosi nchini Canada. Waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau , ambaye alikuwa mwenyeji wa mkutano huo katika mji wa kitalii wa Quebec , aliita ahadi hiyo "uwekezaji mkubwa kabisa katika elimu kwa wanawake na wasichana walioko katika mizozo pia wanaojikuta katika hali ya machafuko."
Fedha hizo ni zaidi ya kundi la wanaharakati wanawake ambalo lilikutana na Trudeau pembezoni mwa mkutano huo lilivyooomba, na kusababisha kundi la G7 kupata kupongezwa na makundi ya kijamii na wanaharakati, ikiwa ni pamoja na mshindi wa nishani ya amani ya nobel Malala Yousafzai ambaye aliyema fedha hizo zitawapa wasichana matumaini zaidi kwamba wanaweza kujenga hali zao za baadaye vizuri zaidi."
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae
Mhariri: Caro Robi