Trump akataa wito wa kutoa ushahidi bungeni
5 Februari 2021Wabunge wa chama cha Democratic katika baraza la wawakilishi wamemtaka Donald Trump kutoa ushahidi chini ya kiapo katika mashtaka ya Baraza la Seneti dhidi yake, kujibu tuhuma kwamba alilichochea kundi la wafuasi wake lililovamia jengo la bunge.
Ingawa Wademocrat wanaweza wasiwe na nguvu ya kulaazimisha ushahidi wa Trump, ombi kutoka kwa wasimamizi wa mashtaka wa baraza la wawakilishi ni sehemu ya juhudi za kuyaweka matukio ya vurugu ya Januari 6 kwenye rekodi ya historia, na kumuajibisha kwa matamshi yake.
Wademocrat watatazamia kutumia kukataa kwake kutoa ushahidi dhidi yake wakati wakihoji kuwa rais huyo mstafu alikwepa kuwajibika kutokana na matendo yake.
Saa kadhaa baada ya kutolewa kwa ombi la Wademocrat siku ya Alhamisi, mshauri wa Trump Jason Miller alipuuza mashtaka hayo na kuyataja kama yasio ya kikatiba, na kwamba rais mstafu hangetoa ushahidi. Katika hatua tofauti, mawakili wa Trump walikosoa ombi hilo walilolitaja kama mkogo. Kesi ya mshtaka inaanza Februari 9.
Trump ambaye ndiye rais wa kwanza kushtakiwa mara mbili, anatuhumiwa kwa kuchochea uasi Januari 6, wakati kundi la wafuasi wake lilipovunja na kuingia kwa nguvu katika jengo la bunge kuvuruga zoezi la kuthibitisha uishindi wa Joe Biden, ambapo watu watano walifariki.
Kabla ya vurugu hizo, Trump aliwaambia wafuasi wake kupambana ili kubadili matokeo ya kushindwa kwake. Jamie Raskin ni msimamizi mkuu wa mashtaka wa baraza la wawakilishi.
"Katika tabia yake akiwa rais wa Marekani, na katika uvunjaji wa kiapo chake cha kikatiba cha kuiendesha ofisi ya rais kwa uaminifu na kadiri ya uwezo wake kuilinda, na kuitetea katiba ya Marekani, na katika ukiukaji wa wajibu wake wa kikatiba wa kuhakikisha sheria zinatekelezwa kwa uaminifu, Donald John Trump alishiriki uhalifu wa kiwango cha juu na makosa madogo madogo kwa kuchochea vurugu dhidi ya serikali ya Marekani," alisema Jamie Raskin, msimamizi mkuu wa mashtaka kwenye baraza la wawakilishi.
Wademocrat wanasema mashtaka hayo ni muhimu kutoa hatua ya mwisho ya uwajibikaji wa shambulizi hilo. Iwapo Trump atatiwa hatiani, Baraza la Seneti litafanya kuira ya pili kumuondolea haki ya kuwania uongezi tena.
Mfuasi wa Trump avuliwa majukumu bungeni
Katika tukio jengine hapo jana, baraza la wawakilishi linalodhibitiwa wa Wademocrat lilipiga kura kumuadhibu mwakilishi wa Republican aliekumbatia dhana za njama na kuidhinisha vurugu.
Mbunge huyo Marjorie Taylor Greene alietuhimiwa kwa kutoa matamshi makali na kuunga mkono kuuawa kwa wabunge wa Democratic, alivuliwa majukumu yake kwenye kamati mbili za bunge za elimu na bajeti.
Adhabu hiyo iliyoungwa mkono na wabunge wa vyama vyote na kupita kwa kura 230 dhidi ya 199, ilitokea saa kadhaa baada ya Greene, mfuasi sugu wa Donald Trump, kusimama bungeni na kulaani vuguvugu la nadharia za njama, na kuelezea masikitiko yake kwa kusambaza taarifa za upotoshaji.
Warepubican 11 walikaidi msimamo wa chama chao na kujiunga na Wademocrat katika kura hiyo ya kumuadhibu Greene, ambaye kabla ya kugombea, alichapisha vidio ambamo alionekana akimnyanyaa mwanafunzi alienusurika katika tukio la ufyatuaji risasi shuleni, na kutilia mashaka mashambulizi ya Septemba 11, 2001.
Chanzo: Mashirika