1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump amteua McMaster kuwa mshauri wa usalama wa taifa

21 Februari 2017

Rais wa Marekani, Donald Trump amemteua Herbert Raymond McMaster kuwa mshauri mpya wa usalama wa taifa, baada ya aliyekuwa anashikilia nafasi hiyo, Jenerali Michael Flynn kujiuzulu.

https://p.dw.com/p/2XxLs
USA Generalleutnant H. R. McMaster und Dnald Trump in Palm Beach
Picha: Reuters/K. Lamarque

''Hivyo nilitaka kutangaza kuwa H.R. McMaster atakuwa mshauri wa usalama wa taifa. Ni mtu mwenye kipaji na uzoefu mkubwa. Kwa siku mbili zilizopita nimepitia na kusoma mambo mengi. Anaheshimika na kila mtu katika jeshi na tunaona heshima kubwa kuwa naye.''

Ni rais wa Marekani, Donald Trump akimtangaza McMaster kuwa mshauri mpya wa usalama wa taifa, wakati akizungumza na waandishi habari jana katika eneo lake binafsi la mapumziko la Mar-a-Lago, huko Florida. Trump amesema amefikia uamuzi huo kutokana na mikutano kadhaa iliyofanyika.

USA Michael Flynn
Michael Flynn aliyejiuzulu kuwa mshauri wa usalama wa taifaPicha: Reuters/C. Barria

Mshauri wa usalama wa taifa ni msaidizi huru wa rais na haitaji kuidhinishwa na Bunge la Marekani. Taarifa ya Ikulu ya Marekani iliyotolewa jana usiku imeeleza kuwa McMaster Luteni wa jeshi, aliyekuwa na majukumu maalum katika vita vya Iraq na Afghanistan amesema anaona fahari kuteuliwa kushika wadhifa huo wa kuwatumika Wamarekani na kwamba usalama wa nchi hiyo kitakuwa kipaumbele chake cha kwanza.

Mtangulizi wa McMaster alijiuzulu kwa upotoshaji

Wiki iliyopita, mtangulizi wa McMaster Jenerali Michael Flynn alilazimika kujiuzulu nafasi hiyo baada ya kumpotosha Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence juu ya mazungumzo kuhusu vikwazo dhidi ya Urusi, aliyoyafanya na balozi wa Urusi nchini Marekani. Hata hivyo katika mkutano wake na waandishi habari Alhamisi iliyopita, Trump alisema amesikitishwa na jinsi Flynn alivyompotosha Pence, lakini haamini kama Flynn alifanya kosa lolote kuwa na mazungumzo hayo.

Uteuzi huo uliofanywa na Trump unafuatia siku kadhaa za mahojiano na mikutano na watu wengine, akiwemo John Bolton na Robert Harward ambaye wiki iliyopita aliukataa uteuzi huo. Trump amesema McMaster atafanya kazi sambamba na aliyekuwa akikaimu nafasi ya mshauri wa usalama wa taifa, Jenerali mstaafu Keith Kellogg.

McMaster, mwenye umri wa miaka 54 ana Shahada ya Uzamifu katika historia ya Marekani aliyoipata kutoka Chuo Kikuu cha North Carolina. Mwaka 2014, alikuwa miongoni mwa watu 100 waliotajwa na jarida la ''Time'' kama watu wenye ushawishi mkubwa. Mbali na kuwa na majukumu muhimu katika vita vya Afghanistan, Iraq na Vita vya Ghuba, McMaster pia anafahamika kutokana na hatua yake ya kukosoa jeshi la Marekani kujihusisha na vita vya Vietnam.

USA Proteste gegen Donald Trump in Los Angeles
Maandamano ya kumpinga Trump, Los AngelsPicha: Reuters/D. McNew

Hayo yanajiri wakati ambapo wanaharakati wanaompinga Trump jana waliitumia siku ya mapumziko ya kuwakumbuka marais waliopita, kufanya maandamano kwenye miji ya Atlanta, Chicago, Los Angeles, Washington pamoja na miji mingine ya Marekani. Polisi inakadiria kuwa kiasi ya watu 10,000 walishiriki katika maandamano yaliyofanyika mbele ya hoteli ya Trump International na karibu na Bustani ya Central Park iliyoko New York.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, AFP, DPA
Mhariri: Iddi Ssessanga