Trump aruhusu kutolewa kwa nyaraka za siri za FBI
3 Februari 2018Hali hiyo inazidisha mapambano kati ya Ikulu ya White House na waendesha mashitaka wanaochunguza kundi la kampeni ya rais.
Trump alikaidi mkurugenzi wake wa FBI na wizara ya sheria na kuamuru kutolewa hadharani waraka wenye kurasa nne wa Republican , ambao unaonesha matumizi mabaya ya madaraka na kuelemea chama kimoja katika shirika hilo kubwa nchini Marekani linalolinda haki.
"Nafikiri ni fedheha. Kile kinachoendelea katika nchi hii, nafikiri ni fedheha," Trump aliyeonekana kuwa katika hali ya kutofurahishwa, alisema wakati akitangaza uamuzi wake wa kuruhusu nyaraka hizo za kumbukumbu kutolewa hadharani. "Watu wengi wanapaswa kuona aibu na zaidi ya hapo."
Wademocrats na baadhi ya Warepublican wamelalamika kuwapo na mchezo mchafu kuhusiana na waraka huo, wakipuuzia kutolewa kwake kuwa ni kama sarakasi tu, na juhudi nyingine dhaifu kuvuruga uchunguzi kuhusiana na mahusiano kati ya timu ya kampeni ya Trump na Urusi.
Wanadai waraka huo , ulioandikwa na Devin Nunes, afisa wa mpito wa Trump, mbunge na mwenyekiti wa kamati ya bunge ya ujasusi, ina matundu makubwa. FBI binafsi imesema ina "wasi wasi mkubwa" na usahihi wa waraka huo.
Kutupiana lawama
Waraka huo unadai kwamba utafiti uliogharamiwa na chama cha Democratic ulisababisha FBI kufanya upelelezi dhidi ya msaidizi wa zamani wa Trump, Carter Page.
Katika taarifa , afisa wa habari wa Ikulu ya Marekani Sarah Sanders alisema waraka huo, "unatoa maelezo yenye wasi wasi mkubwa juu ya kuaminika kwa maamuzi yaliyofanywa katika ngazi ya juu ya wizara ya sheria na FBI.
Mtoto wa kiume wa Trump Don Jr aliandika katika ukurasa wa Twitter kwamba inapaswa kuwa "mchezo umekwisha" kwa uchunguzi wa Urusi.
Uongozi wa Trump wa mwaka mmoja sasa umegubikwa na madai kwamba wasaidizi wake kadhaa, ikiwa ni pamoja na Don Jr na mkwe wake wa kiume Jared Kushner , huenda walishirikiana na serikali ya Urusi kumwangusha mgombea wa chama cha Democratic Hillary Clinton.
Mshauri maalum Robert Mueller tayari amewataja maafisa wawili ikiwa ni pamoja na mwenyekiti wa kampeni ya Trump Paul Manafort , na maafisa wengine wawili kwamba wamekiri kudanganya kwa wachunguzi, ikiwa ni pamoja na mshauri wa zamani wa usalama wa taifa Michael Flynn.
Rais Trump mwenye umri wa miaka 71 amekana madai hayo na kusema ni taarifa za uongo na mpango wa Wademocrat. Mueller anatarajiwa hivi karibuni kumtaka atoe ushahidi chini ya kiapo juu ya kile anachokifahamu.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Yusra Buwayhid