Trump asema hakumrekodi Comey
23 Juni 2017Rais wa Marekani Donald Trump, amesema hakurekodi mazungumzo yake na mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Upelelezi la Marekani, FBI James Comey, kuhusu uchunguzi wa madai kwamba Urusi iliingilia uchaguzi mkuu wa Marekani mwaka uliopita.
Kauli hiyo ameitoa katika ukarasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, ambapo Rais Trump alisema hana aina yeyote ya mazungumzo aliyoyarekodi kati yake na Mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Upelelezi la Marekani, FBI James Comey, ambaye alimfukuza kazi mwezi uliopita na kusababisha mvutano wa kisiasa. Kauli hiyo inatofautiana na ile ya awali aliyoitoa mwezi uliopita baada ya kusema kuwa huenda akawa amerekodi mazungumzo yake na Comey.
Mapema jana Trump alisema hajui iwapo kuna kanda au mazungumzo yoyote kati yake na Comey, yaliyorekodiwa, lakini kwa upande wake yeye hakurekodi. Ingawa mara baada ya kumfukuza kazi Comey, Trump alisema ni bora mkurugenzi huyo wa zamani wa FBI awe na matumaini kwamba hakuna kanda yenye sauti iliyorekodi mazungumzo yao ya awali.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uwezekano wa kuwepo kanda yenye mazungumzo kati ya Trump na Comey, msaidizi katika ofisi ya habari ya Ikulu ya Marekani, Sarah Huckabee Sanders alisema, ''mlitaka awape jibu, na amewapa jibu. Sina taarifa yoyote kuhusu chochote. Nadhani kauli yake inaeleweka wazi.''
Comey alikuwa akiongoza uchunguzi wa madai hayo
Hadi alipofukuzwa kazi, Comey alikuwa akiongoza uchunguzi wa madai kuhusu Urusi kuingilia uchaguzi mkuu wa Marekani mwaka uliopita. Kiongozi huyo wa zamani wa FBI alikiri mbele ya kamati ya Baraza la Seneti kwamba Trump alimtaka aache kumchunguza aliyekuwa mshauri wa usalama wa taifa la Marekani, Michael Flynn baada ya kushutumiwa kwamba alishirikiana na Urusi.
Trump anakabiliwa na mzozo mkubwa unaohusu madai ya kuwepo uwezekano kwamba timu yake ya kampeni ya uchaguzi ilikuwa ikishirikiana kwa karibu na Urusi.
Mkurugenzi wa zamani wa FBI, Robert Mueller hatimaye aliteuliwa na wizara ya sheria, kama mshauri maalum kuongoza uchughuzi huo kuhusu madai hayo dhidi ya Urusi. Akizungumza katika mahojiano yake na kituo cha televisheni cha Marekani cha Fox, Trump alisema Mueller na Comey walifanya kazi pamoja katika wizara ya sheria wakati wa utawala wa rais George W. Bush. Alipoulizwa iwapo Mueller anatakiwa kuacha kufanya uchunguzi huo kutokana na urafiki wake na Comey, Trump alisema itabidi waliangalie suala hilo.
Madai ya kuwepo ushirikiano kati ya timu ya kampeni ya Trump na Urusi yameleta mvutano mkubwa katika miezi mitano ya kwanza ya utawala wa Rais Trump. Kamati ya bunge inayochunguza madai hayo, imeipa Ikulu ya Marekani hadi leo Ijumaa, kuwa imewasilisha kanda zozote zile kama zipo.
Hata hivyo, Urusi imekuwa ikikanusha madai kwamba ilijaribu kuingilia uchaguzi wa Marekani, ikiwemo kudukua barua pepe za maafisa waandamizi wa chama cha Democrat.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP, Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf