Trump atafakari amri mpya ya marufuku dhidi ya wahamiaji
13 Februari 2017Wakati huu ambapo marufuku hiyo imezuiwa na mahakama kuu ya rufani ikisubiri mapitio mengine ya kisheria, Trump "anatafakari na kuangalia kila njia," mshauri wa rais Stephen Miller alikiambia kituo cha televisheni cha Fox News jana Jumapili.
Ikulu ya Marekani inaweza ama kufungua rufaa ya dharura katika mahakama kuu, ikitetea uzito wa amri hiyo katika mahakama za chini ama kutoa amri mpya. Chaguo la mwisho lilitolewa na Trump binafsi siku ya Ijumaa.
"Tunatafakari hatua mpya na za ziada kuhakikisha kwamba uhamiaji sio nyenzo ya kuwaruhusu watu ambao wanauhasama na taifa hili pamoja na maadili yake kuingia nchini," Miller alisema katika kipindi cha televisheni ya NBC kiitwacho "Kutana na wanahabari".
"Hakuna kitu kinachoitwa ukuu wa mahakama. Kile ambacho majaji walifanya ni kuondoa madaraka ambayo yako moja kwa moja mikononi mwa rais wa Marekani.
Mkutano na waziri mkuu wa Canada
Suala hilo ni hakika kwamba litajitokeza wakati rais Trump atakapokutana na waziri mkuu wa Canada Justin Trudeua leo Jumatatu, ambaye alisema baada ya rais huyo kutoka chama cha Republican kutoa amri hiyo ya marufuku kwamba nchi hiyo jirani ya Marekani upande wa kaskazini inawakaribisha kwa mikoni miwili "wale wanaokimbia ukandamizaji , ugaidi na vita."
Wakati hatima ya marufuku ya Trump dhidi ya wakimbizi na wasafiri kutoka mataifa saba yenye Waislamu wengi bado inashikiliwa na mahakama, amri nyingine ya rais inayotaka kurejeshwa makwao wahamiaji ambao hawana hati za ukaazi na hawajaorodheshwa imesafisha njia ya kukamatwa kwa mamia ya watu, wengi wao watu kutoka mataifa ya Amerika ya kusini , wiki iliyopita.
Wakati maelfu ya Wamexico waliandamana jana dhidi ya kiapo cha Trump kwamba atailazimisha nchi hiyo kugharamia ujenzi wa kile alichosema "ukuta mkubwa wa kupendeza,"kati ya Marekani na Mexico, ikulu ya Marekani imethibitisha mipango ya rais kutafakari kuhusu hatua mpya kuharakisha kurejeshwa makwao wahamiaji haramu.
Katika maandamano yaliyofanyika nchini Mexico kulaani hatua za ukandamizaji za rais Trump kwa wahamiaji na kutaka kujenga ukuta mwanasiasa maarufu wa Mexico Andres Manuel Lopez Abrador alisema hatua ya ujenzi wa ukuta ni kinyume na ubinadamu.
"Wakitaka kujenga ukuta kuwatenganisha watu , ama wakati neno "wageni" likitumika kuwatukana, kuwadhalilisha na kwa nia ya ubaguzi dhidi ya binadamu wenzetu, inakwenda kinyume na ubinadamu, ni utovu wa akili na kinyume na historia."
Wakati huo huo Korea ya kaskazini imesema imefanya jaribio lililofanikiwa leo la kombora, na kuzusha wito unaoongozwa na Marekani kufanyika haraka kwa kikao cha baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya jaribio hilo kuonekana kwamba ni changamoto kwa rais Donald Trump.
Muandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Yusuf Saumu