1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump atishia kusitisha msaada kwa Palestina

Caro Robi
3 Januari 2018

Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kusitisha msaada wa thamani ya dola milioni 300 kwa mwaka kwa Palestina, hatua ambayo imeshutumiwa vikali na viongozi wa Palestina wakisema hawatatetereshwa na vitisho. 

https://p.dw.com/p/2qGOt
Mar-a-Lago Trump Video Konferenz
Picha: picture-alliance/Zuma

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Rais Trump, amesena wanawalipa Wapalestina mamilioni ya dola kwa mwaka na hawapati shukran wala heshima kutoka kwao akiongeza kuwa kutokana na kuwa Wapalestina hawana nia tena ya kufanya mazungumzo kuhusu amani basi hakuna haja kuendelea kuwapa misaada katika siku za usoni.

Haijabainika wazi iwapo Trump anatishia kusitisha bajeti nzima kwa ajili ya Palestina ya kima cha dola milioni 319 au la. Afisa mwandamizi wa Palestina Hanan Ashrawi amesema hawatatishwa na Marekani na kumshutumu Rais Trump kwa kuhujumu azma ya Palstina kutafuta amani, uhuru na haki.

Nabil Abu Rdainah, msemaji wa Rais Abbas amesema Jerusalem haiuzwi, si kwa dhahabu wala fedha akiongeza kusema kuwa Wapalestina hawapingi kurejea katika meza ya mazungumzo ya kutafuta amani yaliyokwama mwaka 2014, lakini kwa misingi ya kuundwa taifa la Palestina kuambatana na misingi iliyokuwepo kabla ya Israel kuuchukua kwa nguvu ukingo wa magharibi, Jerusalem Mashariki na ukanda wa Gaza wakati wa vita vya mwaka 1967.

Marekani imekuwa ikiipa mamlaka ya ndani ya Palestina msaada wa kupiga jeki bajetii yake na w kiusalama pamoja na dola nyingine milionii 304 kwa ajili ya miradi ya Umoja wa Mataifa katika ukingo wa magharibi na Gaza.

Protesten im Westjordanland
Waandamanaji wakivikimbia vikosi vya Israel wakati wa maandamano ya kumpinga TrumpPicha: Reuters/M. Qawasma

Waziri wa utamaduni wa Israel Miri Regev, mwanachama wa chama cha Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu cha Likud amesema amefurahishwa na kauli ya Trump ya kutaka kuikatia Palestina misaada, akisema ni wakati kukoma kuiambia Palestina maneno matamu.

Lakini Tzipi Livni, mwanasiasa wa upinzani wa Israel na mjumbe wa zamani wa kusimamia mchakato wa amani amesema serikali inayojitizama liyowajibika na iliyokamaa ya Israel inapaswa kumueleza Trump kuwa ni kwa maslahi ya Israel kuzuia mzozo wa kibinadamu Gaza na kuendelea kufadhili vikosi vya usalama vya Palestina vinavyoshirikiana na Israel.

Trump aliingia madarakani akijivuna kuwa ataweza kufikia makubaliano madhubuti kuhusu mzozo wa muda mrefu wa Mashariki ya kati, jambo ambalo limewashinda watangulizi wake tangu miaka ya sitini.

Kwa takriban nusu karne Marekani imekuwa mpatanishi mkuu wa mchakato wa kutafuta amani kati ya Israel na Palestina, lakini vitendo vya Trump kama kutishia kusitisha misaada kwa Palestina na kutambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel mwezi uliopita unatilia shaka iwapo ataweza kufikia lengo la kupatikana amani Mashariki ya Kati.

Rais wa Mamlaka ya ndani Mahmud Abbas amesema Marekani haistahili tena kuwa mpatanishi wa mzozo wa Mashariki ya Kati kutokana na uamuzi wa Trump wa kutambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel.

Palestina imeitaka Marekani kama kweli ina nia ya kupatikana amani katika kanda hiyo basi sharti iheshimu taratibu na misingi.

 

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters/AP

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman