Trump aweka mashariti mkutano na Kim wa Korea kaskazini
10 Machi 2018Kukubali kwa Trump siku ya Alhamis mwaliko wa Kim kukutana nae, bila masharti ya awali, kumekuja kwa mshituko kwa sehemu kubwa ya jumuiya ya kimataifa. Hakuna rais wa Marekani aliyeko madarakani aliyekutana na kiongozi wa taifa hilo lenye usiri.
"Mkutano huu hautafanyika hadi pale tutakapoona hatua kamili ambazo zinakwenda pamoja na maneno na malumbano ya Korea kaskazini," mkuu wa masuala ya mawasiliano wa Ikulu ya Marekani White House Sarah Sanders amesema jana Ijumaa (09.03.2018).
Sanders amedokeza kwamba Marekani haijafanya maridhiano yoyote na Korea kaskazini , wakati Korea kaskazini imetoa ahadi kubwa, kuweza kuachana na mpango wake wa kinyuklia na kuachana na hatua yake ya kufanya majaribio ya makombora na kukubali kwamba luteka ya kila mara ya kijeshi kati ya Marekani na Korea kusini itaendelea.
Trump ana matumaini kwamba hatua zaidi zinaweza kupigwa, Sanders alisema, na kwa wakati huu, Marekani haitaacha kuendelea kuweka mbinyo dhidi ya Korea kaskazini ili kufikisha mwisho mpango wake wa kinyuklia. Jioni ya jana Ijumaa Trump alisema , makubaliano yako "karibu sana kupatikana."
Makubaliano mazuri kwa dunia
"Makubaliano hayo na Korea kaskazini yanatayarishwa na yatakuwa , kama yatakamilika, mazuri sana kwa dunia," Trump aliandika katika ukurasa wa Twitter, akimaanisha kwamba Korea kaskazini inaachana na silaha zake za kinyuklia. "Muda na mahali pataamuliwa," aliongeza.
Mkutano baina ya kiongozi wa Marekani na Korea kaskazini unaweza kuwa fursa ya mafanikio katika miongo kadhaa ya juhudi za kurejesha amani katika rasi ya Korea.
Mualiko wa Kim unafuatia hatua kadhaa za kidiplomasia , zinazoonekana na wachunguzi wengi na vyombo vya habari kuwa kama "hatua za kuvutia" zilizounganishwa na kuhudhuria kwa Korea kaskazini katika mashindano ya olimpiki ya majira ya baridi mjini Pyeongchang mwezi uliopita. Chung Eui Yong, ambaye aliongoza ujumbe wa Korea kusini kukutana na na Kim mjini Pyongyang mapema wiki hii, alikuwa wa kwanza kutangaza kukubali kwa Trump mwaliko huo.
Kiongozi wa Korea kaskazini , alieleza "kuwapo kwake tayari " kukutana na Trump, na Trump atakutana na Kim mwezi Mei "ili kufanikisha kuondolewa kwa silaha za kinyuklia kabisa;" Chung aliwaambia waandishi habari. Maafisa wa Korea kusini walifikisha mwaliko huo kutoka kwa Kim siku ya Alhamis wakati walipouarifu utawala wa Trump kuhusiana na mazungumzo ya hivi karibuni kati ya Korea mbili.
Licha ya wachambuzi wengi kuona hatua hizo kama ni mabadiliko ya kushangaza, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Rex Tillerson alisema Trump kukubali mwaliko , "sio jambo la kushangaza bila shaka." Ripoti kutoka kwa Wakorea kusini zinaonesha "hamasa kubwa " kutoka kwa Kim kutaka kuzungumza na Marekani, Tillerson alisema.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae
Mhariri: Bruce Amani