1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump agusia suluhu la amani kwa mzozo wa Korea Kaskazini

Daniel Gakuba
7 Novemba 2017

Rais wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa Korea Kusini Moon Jae In wameafikiana kutafuta suluhisho la amani katika mzozo wa nyuklia wa Korea Kaskazini bila hata hivyo kuondoa uwezekano wa matumizi ya nguvu za kijeshi.

https://p.dw.com/p/2nA9v
Südkorea Donald Trump und Moon Jae-in
Rais Donald Trump na mwenzake wa Korea Kusini Moon Jae-in mjini SeoulPicha: Reuters/J. Ernst

Azma ya viongozi hao wawili imetangazwa katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari uliofanyika muda mfupi uliopia mjini Seoul. Rais wa Korea Kusini Moon Jae In amesema amekubaliana na Rais Trump kuitolea wito Korea Kaskazini kuja kwenye meza ya mazungumzo, kwa ahadi ya kusaidiwa kupata mustakabali wenye matumaini. Rais Donald Trump pia amethibitisha kupatikana kwa maendeleo katika mchakato huo, akisifu mchango wa China na kuzitaka nchi nyingine kusaidia.

Amesema, ''China inafanya juhudi kubwa kulitatua tatizo hili la Korea Kazini, na tuna matumaini kuwa Urusi pia itasaidia. Na kama mnavyofahamu, tumeanzisha mazungumzo na nchi nyingine nyingi na tuna uhakika kwamba zimeanza kujaribu.'' Trump ameendelea kueleza kuwa ''tukipata China na Urusi pamoja na nchi nyingine, tunaamini suluhisho litapatikana, tena haraka.''

Lakini licha ya matumaini hayo ya kupatikana suluhisho la kidiplomasia, Trump vile vile ameionya Korea Kaskazini, akisema Marekani iko tayari kutumia uwezo wake mkubwa wa kijeshi kujilinda na kuwalinda washirika wake kama hatua hiyo itahitajika. Rais wa Korea Kusini amejizuia kutoa kauli yoyote inayohusisha hatua za kijeshi katika kusuluhisha mgogoro katika ras ya Korea, lakini amesema watatumia njia zote zinazowezekana kuizuia Korea Kaskazini kuharibu maendeleo yaliyofikiwa na nchi yake.

Suluhisho lazima lipatikane

Trump ambaye anasindikizwa na mkewe Melania amewasili nchini Korea Kusini asubuhi ya leo akitokea Japan, na kabla ya mazungumzo na waandishi wa habari amezuru kambi ya jeshi ya Humphreys, ambayo ndio kituo kikubwa cha jeshi la Marekani nchini Korea Kusini.

Südkorea Präsident Donald Trump bei seiner Ankunft in Seoul
Ziara ya Trump Korea Kaskazini, inaweza kuzidisha mvutano na Korea KaskaziniPicha: picture-alliance/AP Photo/Lee Jin-man

Akizungumza na makamanda wakuu wa kambi hiyo, Trump amesema na hapa nanukuu, '' Hatimaye suluhisho litapatikana, suluhisho hupatikana mara zote, na ni lazima lipatikane''. Hata hivyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu suluhisho alilokuwa akilimaanisha.

Rais huyo wa Marekani amemsifu mwenzake wa Korea Kusini kwa kumpa ushirikiano mkubwa, ingawa inafahamika kuwa viongozi hao wana mitazamo tofauti juu ya masuala muhimu, yakiwemo namna ya kuushughulikia mzozo wa nyuklia wa Korea Kaskazini, na hali ya biashara baina ya Marekani na Korea Kusini.

Kuzidi kwa mvutano

Kombi-Bild  Trump und Kim Jong Un
Donald Trump na Kim Jong-un wamekuwa wakitoleana lugha ya matusiPicha: Reuters/K. Lamarque/KCNA

Ziara ya Trump nchini Korea Kusini imefanyika kukiwa na mvutano mkubwa kati ya Korea Kaskazini kwa upande mmoja, na Marekani na washirika wake, hasa Kora Kusini na Japan kwa upande mwingine, kutokana na mfululizo wa majaribio ya makombora na zana za atomiki ambayo yamekuwa ya kifanywa na Korea Kaskazini, na ubadilishanaji wa lugha ya matusi baina ya Rais Donald Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un.

Korea Kusini ni nchi ya pili kwenye orodha ya nchi tano ambazo Trump atazizuru katika ziara yake hii barani Asia. Aliwasili akitokea Japan, na hapo kesho atawasili nchini China. Baadaye ataendelea hadi Vietnam na Ufilipino.

Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae, ape, rtre

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman