1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump kuamua kuhusu hatua ya kijeshi Syria

10 Aprili 2018

Rais wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kuamua kama atachukua hatua za kijeshi dhidi ya utawala wa Syria baada ya kuapa kujibu kwa nguvu shambulizi la karibuni linalodaiwa kuwa la sumu nchini humo.

https://p.dw.com/p/2vlBM
USA Präsident Donald Trump im Weißen Haus in Washington
Picha: picture-alliance/CNP/MediaPunch/J. LoScalzo

Marekani iliwasilisha jana rasimu ya azimio kufuatia madai ya shambulizi la gesi ya sumu katika mji wa Douma unaodhibitiwa na waasi ambalo limewaua karibu watu 40. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley aliwaambia wajumbe wa Baraza la Usalama kuwa Marekani inataka azimio hilo lipigiwe kura, ijapokuwa Urusi inasema lina vipengele visivyokubalika. Urusi iliwasilisha pendekezo lake mwezi Januari ambalo limekataliwa na mataifa ya Magharibi yanayosema kuwa linaweza kuipa serikali ya Syria faida kubwa kuhusiana na uchunguzi unaofanywa ndani ya nchi. Watalaamu wanakutana ili kujadili rasimu za maazimio hayo.

Juhudi za Marekani kutaka uchunguzi kufanywa zimekuja wakati kukiwa na mvutano kuhusu uwezakano wa hatua ya kijeshi nchini Marekani, huku Trump akisema maamuzi muhimu yatachukuliwa katika saa 48. "Tutafanya uamuzi leo usiku, au muda mfupi baadae na utasikia kuhusu uamuzi huo, lakini hatuwezi kuyafumbia macho maovu tuliyoyaona sote. Hasa wakati tukiwa na uwezo. Kwa sababu ya nguvu za Marekani, tunaweza kuzuia unyama huo"

USA Sitzung des UN-Sicherheitsrats in New York
Baraza la Usalama liliitisha kikao cha dharuraPicha: Reuters/B. McDermid

Wakati wa mkutano wa jana Baraza la Usalama ambapo ulishuhudia vita vikali vya maneno, balozi wa Urusi Vassily Nabenzia alionya kuwa shambulio la kijeshi nchini Syria linaweza kusababisha madhara makubwa na akasisitiza kuwa bado hakuna ushahidi kuwa kemikali aina ya Klorini au sarin ilitumika katika shambulizi la Jumamosi mjini Douma "Tunawaomba wanasiasa wa nchi za Magharibi kuyapunguza maneno matupu na kuanza kutafakari uwezekano wa kutokea madhara na kukomesha ueneaji wa vitisho hivyo kwa usalama wa dunia"

Haley amelitaka baraza hilo kuchukua hatua, lakini akaonya kuwa Marekani iko tayari kujibu, hata bila ya ridhaa ya Umoja wa Mataifa "Tumefikia wakati ambapo dunia lazima ione haki ikitendeka. Historia itaonyesha huu kuwa wakati ambapo baraza la usalama lilitekeleza wajibu wake au lilishindwa kabisa kuwalinda watu wa Syria". Urusi imetumia nguvu yake ya turufu mara 11 katika baraza hilo ili kuzuia hatua zozote zinazoilenga Syria ambayo ni mshirika wake

Wakati huo huo, mkuu wa shirika la haki za binaadamu la Syria amesema wanajeshi wa Syria na washirika wake wamewekwa katika hali ya tahadhari kote nchini humo na kuondoka katika baadhi ya vituo vyao vya kijeshi kutokana na uwezekano wa kufanyika mashambulizi ya kigeni.

Wanaharakati katika mkoa wa mashariki wa Deir al-Zour wamesema wanajeshi wa Syria na washirika wao wamehama kutoka vituo vya ukaguzi vya kijeshi.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga