1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump kutangaza sera mpya dhidi ya Cuba

16 Juni 2017

Rais wa Marekani, Donald Trump, leo anatangaza mabadiliko ya sera kuhusu Cuba ambapo anatarajiwa kuyazuwia makampuni yanayofanya biashara ya kijeshi na Cuba pamoja na kuimarisha sheria za usafiri kuelekea kisiwa hicho.

https://p.dw.com/p/2enIL
Kuba - Tourismus  - USA
Picha: picture alliance/EFA/O. Barria

Hayo yatakuwa ni kubadili sera ya kujongeleana kati ya Marekani na Cuba ilioanzishwa na Rais Barack Obama mnamo miaka ya mwisho kabla ya kuondoka madarakani.

Rasimu ya mipango hiyo ya rais iliyotolewa jana jioni na Ikulu ya Marekani imeeleza kuwa sera hizo mpya zimeandaliwa kwa ajili ya kuwawezesha watu wa Cuba. Taarifa hiyo imeeleza kuwa sera hiyo haiwalengi watu wa Cuba, bali utawala wa Cuba na kuongeza kuwa lengo lake ni la uhuru wa kisiasa na kidini pamoja na kuheshimu haki za binaadamu.

USA PK Präsident Donald Trump nach Schießerei in Alexandria, Virginia
Rais Donald TrumpPicha: picture alliance/abaca/O. Douliery

Rais Trump anatarajiwa kutangaza sera hizo mpya mjini Miami, ambako ni makaazi makuu ya jumuiya ya Wacuba wanaoishi uhamishoni nchini Marekani ambao wanaupinga utawala wa kisiwa chao.

Katika miaka yake ya mwisho madarakani, rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama alianzisha juhudi za kidiplomasia za kujihusisha tena na adui yake huyo wa zamani wakati wa Vita Baridi, iliyohusisha kurejesha uhusiano na kuzifungua tena balozi zake. Sera hiyo itaendeleza uhusiano wa kidiplomasia na kuyaruhusu mashirika ya ndege ya Marekani pamoja na meli kuendelea kutoa huduma zake katika kisiwa hicho.

Marekani kuzuwia fedha zake kumiminwa Cuba

Maafisa wa Marekani wamewaambia waandishi habari kwamba Trump atatangaza marufuku katika utowaji wa fedha kwa jeshi la Cuba ambalo limekuwa likijitanua ili kuisaidia sekta ya utalii pamoja tawi lake la kampuni inayohusika na biashara ya zana za kijeshi linalojulikana kama GAESA, ambayo inamiliki hoteli kubwa pamoja na maduka makubwa ya rejareja na makampuni ya kukodisha magari nchini humo. Inakadiriwa kuwa kampuni ya GAESA inachangia zaidi ya nusu ya mapato yanayotokana na biashara nchini Cuba.

Kulingana na sera hizo mpya, Rais Trump pia anatarajiwa kutangaza vikwazo vikali zaidi dhidi ya Wamarekani wanaosafiri kwenda nchini Cuba. Raia wa Marekani bado wataendelea kutumia ndege za kibiashara kwenda Cuba, lakini ikiwa wana sababu 12 tu muhimu, kuanzia shughuli za uwandishi wa habari na elimu, ambazo zitawekewa masharti zaidi pamoja na kupitia makundi yaliyotambuliwa.

Kuba - Tourismus  - USA
Watalii wakiwa Havana, CubaPicha: picture alliance/EFE/A. Ernesto

Jan Erik ni mmoja wa watalii wa Marekani, ''naam natumaini kutokana na uzoefu wangu nchini Cuba, kwamba tutaendelea kuwa na fursa ya kusafiri duniani, ikiwa ni pamoja na Cuba. Ninaamini ni fursa kubwa sana kwa watu wanaoishi hapa kukutana na Wamarekani na kusaidia katika uchumi.''

Hata hivyo, wakosoaji wanasema kuwa mipango hiyo haitauathiri sana kiuchumi utawala wa Cuba na itakipa kisiwa hicho nafasi mpya ya kujitangaza kuwa ni mhanga wa uchokozi wa Marekani na kuwa sababu ya kuahirisha mageuzi ya kidemokrasi.

Mnamo siku ya Jumatano, Cuba ilitangaza kuwa itafanya uchaguzi wa manispaa mwezi Oktoba. Rais Raul Castro alitangaza kuwa ataachia madaraka mwezi Februari mwaka ujao, mwishoni mwa kipindi chake cha pili cha miaka mitano, lakini ameonyesha dalili kuwa ataendelea kuwa mwenyekiti wa chama  tawala cha Kikomunisti, ambacho ni chama pekee kinachoruhusiwa nchini Cuba.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP, http://bit.ly/2sGjdgu
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman