Trump na Kim watia saini makubaliano ya kihistoria
12 Juni 2018Viongozi hao walikamilisha siku ya kihistoria ambayo ilishuhudia viongozi hao wawili wakikutana kwa mara ya kwanza kabisa.
Katika mkutano huo Trump ameahidi kuipatia Korea kaskazini uhakikisho wa usalama wake pamoja na kutangaza katika mkutano na waandishi habari baadaye kwamba Marekani na Korea kusini zitaacha luteka ya pamoja ya kijeshi kama Korea kaskazini inavyodai.
Katika waraka wenye vipengee vinne, Marekani na Korea kaskazini zimeazimia kuweka uhusiano mpya kati ya nchi hizo mbili, kujenga utawala imara na endelevu kuelekea amani akisisitiza azimio la Panmunjeom kutoka Aprili 27.
Katika mkutano na waandishi habari leo rais Donald Trump wa Marekani amesema kwamba jeshi la Marekani litaacha kufanya mazowezi ya pamoja na Korea kusini yakiilenga Korea kaskazini, akisema yanaongeza hali ya wasi wasi na kuyasitisha kutasaidia kuhifadhi fedha nyingi zinazotumika katika mazowezi hayo. Pia amesema atamwalika kiongozi wa Korea kaskazini katika ikulu ya marekani White house na kwamba binafsi angependa kutembelea mji mkuu wa Korea kaskazini Pyongyang.
Nchi hizo mbili hufanya mazoezi ya kijeshi kila mwaka ambayo yanaikera Korea kaskazini , ambayo imekuwa kwa muda mrefu ikidai kutishwa kwa mazowezi hayo na mara nyingi hujibu kwa kuchukua hatua zake, na kusababisha kuongezeka kwa hali ya wasi wasi.
Kim amshukuru Trump
Wakati wa kutia saini makubaliano hayo kati ya Trump na Kim leo asubuhi, rais Trump alisema pande zote mbili zimefurahi kutia saini makubaliano hayo.
"Tunatia saini waraka muhimu sana, waraka ambao una maelezo mapana. na tutajadili hili kwa kina. Kwa hivi sasa naamini mtapata nakala kwa niaba ya mwenyekiti Kim na mimi. Na wote tunafahari kubwa kutia saini waraka huu. Asante."
Kwa upande wake kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un alimshukuru rais Trump kwa kukubali kufanyika mkutano huo.
"Leo tulikuwa na mkutano wa kihistoria na kuamua kuacha nyuma yaliyopita. Na tuko tayari kutia saini waraka huu wa kihistoria. Dunia itaona mabadiliko makubwa. Napenda kueleza shukurani zangu kwa rais Trump kwa kufanikisha mkutano huu. Asante.
Kuhusu vikwazo dhidi ya Korea kaskazini rais Trump amesema kwa hivi sasa vikwazo hivyo vitaendelea , lakini anaangalia uwezekano wa kuviondoa.
Rais wa Marekani amesema pia kwamba kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un ana nia thabiti ya kuharibu kabisa maeneo ambayo nchi hiyo inafanyia majaribio silaha zake.
Kwa upande mwingine waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe na mwenzake wa Malaysia mahathir Mohammed wamekubaliana leo kufanyakazi kwa pamoja kupambana na mipango ya kinyuklia na makombora ya Korea kaskazini. Viongozi hao wamesema wanataka kutuma ujumbe mkali kwa Korea kaskazini kuhusu suala hilo. Waliysema hayo katika mkutano na waandishi habari kufuatia mkutano wao mjini Tokyo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae /rtre
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman