Zuma ataka matokeo ya uchaguzi yatangazwe.
9 Aprili 2008
Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai amesema leo kuwa atatumia fursa ya mikutano na viongozi wa kusini mwa afrika kuwataka viongozi hao wasaidie kuepuesha maafa nchini Zimbabwe.
Akizungumza katika mahojiano na radio ya Afrika Kusini kiongozi huyo wa chama cha upinzani MDC ameeleza kuwa halitakuwa jambo la manufaa kwa nchi za kusini mwa Afrika ikiwa nchi jirani-itakuwa na mgogoro.
Bwana Tsvangirai ameeleza hayo baada ya mazungumzo yake na rais wa Botswana Ian Khama.
Baada ya kuzitembelea Botswana,na Afrika Kusini bwana Tsvangirai anatarajiwa pia kufanya ziara nchini Zambia na Msumbiji.
Wakati huo huo jumuiya ya kimataifa imeimarisha shinikizo kutaka matokeo ya uchaguzi uliofanyika tarehe 29 mwezi uliopita yatangazwe nchini zimbabwe.
Kiongozi wa chama kinachotawala nchini Afrika Kusini ANC bwana Jacob Zuma amejiunga na kampeni ya kutaka matokeo ya uchaguzi wa Zimabwe yatangazwe.Lakini tume ya uchaguzi imesema haitatoa matokeo hayo.
Mwanasheria wa tume hiyo amesema leo kwamba itakuwa hatari kwa mahakama kuu kuamrisha kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa rais.
Mwanasheria huyo George Chikumbirike amekataa kusema ni hatua gani ya matayarisho iliyofikiwa na tume ya uchaguzi katika kutangaza matokeo.Amesema habari hizo ni istihaki ya tume ya uchaguzi na itatangaza itakapokuwa tayari kufanya hivyo.