1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya uchaguzi ya Tanzania yataja baadhi ya wagombea urais

25 Agosti 2020

Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania NEC, leo imeanza zoezi la uteuzi wa wagombea wa nafasi za urais, ubunge na udiwani, ambapo tayari hadi sasa wagombea wanne wa nafasi ya urais wamethibitishwa kukidhi vigezo.

https://p.dw.com/p/3hT5t
Tansania Dodoma | Wahlkampf | CCM Partei
Picha: DW/S. Khamis

Rais John Magufuli anakuwa mgombea wa kwanza kuwasili katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi mjini Dodoma akiambatana na mgombea mwenza ambae pia ni makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, wakiwa na dhima moja kurejesha fomu za kuwania nafasi ya urais walizochukua takriban wiki mbili zilizopita, ilii kuwania kipindi kingine cha miaka mitano kwa mujibu wa katiba ya taifa hili la Afrika Mashariki.

Wakikabidhi fomu hizo kwa NEC wamesema, wamekamilisha vigezo vyote vilivyotakiwa kwa mujibu wa sheria ikiwemo, idadi ya wadhamini kutoka mikoa 10 isipokuwa wameongeza mikoa mitano kama ziada hatua ambayo inaongeza idadi ya wadhamni kutoka ile 2,000 wanaohitajika kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi.

Mkurugenzi wa NEC amesema uhakiki wao umethibitishwa vyema

Äthiopien Tundu Lissu in Dar es Salaam
Mgembea wa chama cha CHADEMA-Tundu LissuPicha: DW/S. Khamis

Akiwasilisha kwa mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi fomu hizo mkurugenzi wa NEC Dokta Charles Mahera amesema, wasimamizi wa uchaguzi wamethibitisha majina ya wadhamini ambao ni wapiga kura katika maeneo ambayo wagombea walifika kwa ajili ya kuomba udhamini.

Kando na mgombea wa chama tawala Dokta John Magufuli kufuzu kuteuliwa na tume ya uchaguzi nchini wengine ni chama cha kilichojipambanua kipagania maslahi ya wafanyakazi na wakulima NRA pamoja na ADA TADEA ambapo kupitia mgombea urais wa chama hicho John Shibuda amesema mbali na ungwe hii kukamilika amewataka wasimamizi wa uchaguzi kusimamia uchaguzi kulingana na katiba na si matakwa ya watu binafsi.

Soma zaidi: NEC yasema maandalizi ya uchaguzi Tanzania yaendelea vyema

Ikiwa zimesalia saa chache kukamilika kwa zoezi la kuwapitisha wagombea urais takriban vyama kumi na tatu bado havijathibithishwa wagombea wake wa nafasi ya urais na NEC endapo wamekidhi vigezo, ambapo hadi sasa vyama vilivyowasili katika ofisi za tume hiyo vikisubiri kuthibithishwa ni pamoja na chama kikuu cha upinzani Chadema, NCCR Mageuzi pamoja na chama cha wananchi CUF.