Tume ya ukweli yaanza kazi Gambia
8 Januari 2019Tume ya ukweli katika taifa dogo la Afrika magharibi la Gambia imeanza kusikiliza ushahidi wakati ikianza uchunguzi kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa na utawala wa Yahya Jammeh.
Ikiwa katika mtindo wa uchunguzi uliofanyika nchini Afrika Kusini katika enzi ya ubaguzi wa rangi, tume hiyo itasikiliza ushahidi kuhusiana na utawala wa miaka 22 wa Jammeh uliokuwa wa ukandamizaji na kuishia mwaka 2016 baada ya kulazimishwa kuondoka madarakani.
Rais Adama Barrow ameisifu tume hiyo kuwa ni hatua kuelekea katika kulipknya taifa hilo na njia ya kuwafikisha mahakamani wale waliohusika na kufikisha mwisho madhila ya wahanga na familia.
Watetezi wa haki za binadamu wanaushutumu utawala kwa kufanya utesaji dhidi ya wapinzani na waandishi habari, mauaji holela, kukamatwa na kuwekwa kizuwizini na kupotea kwa watu katika taifa hilo la Afrika magharibi.