1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tundu Lissu na harakati za "mwanzo mpya" Tanzania

25 Januari 2023

Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu amekamatwa mara kadhaa, kunusurika jaribio la mauaji na kuishi uhamishoni kwa zaidi ya miaka mitano. Lakini sasa amerudi nyumbani "kuandika ukurasa mpya" kwa nchi yake.

https://p.dw.com/p/4MgMY
Tansania Tundu Lissu
Picha: Eric Boniface

Tundu Lissu, wakili mwenye umri wa miaka 55, alierejea nyumbani kwa kipindi kifupi kuwania urais mwaka 2020, amerudi tena kwenye ardhi ya Tanzania akitokea uhamishoni nchini Ubelgiji "kuandika ukurasa mpya" kwa nchi yake.

Alitangaza kuwa angerudi baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuondoa marufuku dhidi ya mikutano ya hadhara ya kisiasa iliyowekwa na mtangulizi wake John Magufuli, ambaye utawala wake wa chuma uliminya upinzani na uhuru wa kujieleza katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

"Kwa kuondolewa kwa marufuku haramu ya shughuli za kisiasa, sasa ni wakati wa kurejea nyumbani na kurejea kazini!" Lissu, wa chama kikuu cha upinzani cha Chadema, alisema kwenye Twitter akitangaza mipango yake ya kurudi nyumbani.

Soma pia: Tundu Lissu arejea Tanzania kutoka uhamishoni

Lissu ambaye ni mkosoaji mkali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mara ya mwisho alikuwa Tanzania mwaka 2020 kushiriki uchaguzi wa Oktoba dhidi ya Magufuli, ambaye alifariki dunia miezi mitano tu baada ya kushinda muhula wake wa pili.

Ushindi wa Magufuli -- kwa asilimia 84 ya kura -- ulibishaniwa vikali na upinzani ukaitisha maandamano.

Tansania Tundu Lissu
Naibu Mwenyekiti wa chama cha upinzani cha CHADEMA cha nchini Tanzania, Tundu Lissu akiwapungia wafuasi wa chama hicho wakati akiwa njiani akitokea uwanja wa ndege jijini Dar es Salaam, Januari 25, 2023.Picha: Eric Boniface

Sababu za kukimbilia uhamishoni

Mara baada ya uchaguzi huo, Lissu alisema alianza kupokea vitisho vya kuuawa na alikamatwa lakini alitafuta hifadhi kwa wanadiplomasia wa kigeni kabla ya kutoroka nchini.

Lissu anatembea kwa kulega kidogo baada ya kupigwa risasi 16 katika shambulio la mwaka 2017 ambalo anaamini lilichochewa kisiasa, na kuhitaji kufanyiwa upasuaji takribani mara 20.  

Soma pia: Rais Samia akutana na Tundu Lissu Ubelgiji    

Tayari alikuwa amekamatwa mara sita mwaka huo, na kisha, Septemba, alipotoka nje ya nyumba yake mjini Dodoma, watu wenye silaha walilimiminia risasi gari lake.

"Lazima ufahamu ukweli kwamba... viungo vyangu vyote, miguu yangu, kiuno changu, mikono yangu, tumbo langu kimsingi lilipasuliwa kwa risasi 16 na hivyo kunirekebisha, kunirudisha kwenye miguu yangu, ilichukua muda mrefu," Lissu aliiambia AFP kabla ya uchaguzi wa 2020.

Lissu alizaliwa mwaka 1968 katika kijiji kidogo kiitwacho Mahambe mkoani Singida, ambapo alisaidia familia yake kulima na kuchunga ng'ombe za baba yake akiwa kijana mdogo, huku akisoma shule ya msingi.

Tansania Tundu Lissu
Tundu Lissu akisalimiana na wafuasi wake baada ya kuwasili Dar es Salaam, Januari 25, 2023.Picha: Eric Boniface

Ni wakati wa kusikiliza vipindi vya redio kuhusu matukio ya sasa na kusoma kwa uchungu ndipo Lissu alipopata ladha ya siasa. Alisomea sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na haraka akatumbukia katika sheria za haki za binadamu na mazingira.

Safari yake ya kisiasa

Alifanya kazi kuanzia 1999-2009 katika Timu ya Wanasheria wa Mazingira (LEAT), akipigania haki za maskini, jumuiya za vijijini, iwe dhidi ya ufugaji wa kamba wa viwandani au makampuni ya kigeni ya kuchimba dhahabu.

Soma pia: Lissu kurejea Tanzania kudai katiba mpya

Pia alifanya kazi katika masuala ya mazingira kati ya 1999 na 2002 kwa Taasisi ya Rasilimali za Dunia yenye makao yake Washington DC (WRI).

Peter Veit wa WRI, ambaye amemfahamu Lissu kwa takriban miongo mitatu, alimtaja kuwa ni mtetezi asiye na woga na asiyekubali kuegemea upande. "Haogopi mtu yeyote. JAmbo analitaja vile lilivyo, na anapata matatizo," Veit aliiambia AFP.

"Yeye ni rasilimali kubwa kwa Tanzania... Ana shauku sana kuhusu nyumba yake na nchi yake na anajaribu kurekebisha mambo nchini Tanzania -- kuhakikisha kuwa kuna mfumo wa kidemokrasia wa uaminifu na uwajibikaji."

Tansania Tundu Lissu
Wafuasi wa chama cha CHADEMA wakiserebuka baada ya kumpokea naibu mwenyekiti wa chama chao Tundu Lissu.Picha: Eric Boniface

Harakati za Lissu zilimpelekea kujiunga na siasa na alichaguliwa mbunge mwaka 2010, na kupanda ngazi hadi kuwa kiongozi wa pili ndani ya chama cha Chadema.

Wakati alikamatwa chini ya serikali iliyopita kuhusiana na harakati zake kaktika sekta ya madini, ilikuwa tu baada ya kuchaguliwa kwa Magufuli alipozidi kupaza sauti, akimtaja rais kama dikteta uchwara na kulaani mazingira ya hofu yaliokuwepo wakati huo.

"Rais Samia Suluhu Hassan, kupitia serikali yake na chama, wameonyesha kuwa wako tayari kwa ajili ya safari mpya. Tunahitaji kuonyesha kwamba sisi pia tuko tayari kwa hilo," alisema Lissu wiki iliyopita.

"Nakuja nyumbani kwa ajili ya mwanzo mpya wa taifa letu."

Chanzo: AFPE