Tunisia, Schulz na AfD Magazetini
14 Februari 2017Tunaanzia Tunisia, chimbuko la vuguvugu la mageuzi ya kidemokrasia katika nchi za kiarabu. Waziri mkuu Youssef Chahid yuko ziarani nchini Ujerumani na atazungumza na kansela Angela Merke. Matumaini ya wananchi katika nchi hiyo ya Afrika kaskazini yamefifia linaandika gazeti la " Reutlinger General Anzeiger" : Tunisia ilikuwa ikisifiwa kuwa nchi pekee ya kidemokrasi katika eneo la Afrika kaskazini tangu vuguvugu la msimu wa kiangazi lilipopiga katika nchi za kiarabu. Lakini kile ambacho kilitia moyo na kumfurahisha mtu kimechukua sura nyengine kabisa. Idadi ya wasiokuwa na kazi nchini Tunisia imepindukia asili mia 15. Hali hiyo imeathiri uchumi na kuzidisha hasira za wananchi. Bila ya shaka Ujerumani ingependelea kuisaidia nchi hiyo ndogo ya bahari ya kati ili kuinusuru demokrasia. Lakini kwanza Ujerumani ingependelea kuiona nchi hiyo ikikubali kuwapokea raia wake walioingia humu nchini kinyume na sheria. Na hayo kansela Angela Merkel atamwambia kinaga ubaga waziri mkuu Youssef Chahid atakapokutana nae mjini Berlin.
CDU/CSU waatapa tapa
Chama kidogo katika serikali kuu ya muungano mjini Berlin, Social Democrats kinazidi kujivunia imani ya wapiga kura tangu walipomteuwa Martin Schulz kugpombea kiti cha kansela uchaguzi mkuu utakapoitishwa septemba mwaka huu. Hali hiyo inawatia kishindo wafuasi wa vyama ndugu vya CDU/CSU wanaohofia mgombea wao, kansela Angela Merkel asije akashindwa kugombea mhula wa nne. Mjadala umehanikiza na mbinu kubiniwa vipi kumtia ila Martin Schulz. Gazeti la "Die Rheinpflaz" linaandika: "Bila ya shaka ni sawa kuhakikisha tuhuma zinazotolewa dhidi ya Martin Schulz zinachunguzwa. Kwamba mshauri wake mkubwa kila wakati alikuwa kazini Berlin na kwamba katika kazi yake ya mjini Berlin daima alikuwa ziarani nchi za nje, hilo haliwezi kuangaliwa kuwa kinyume na sheria, japo kama linagharimu fedha nyingi za walipa kodi. Vyama ndugu vya CDU/CSU vinamwandama na kutaka kumtia ila Martin Schulz. Na hilo halijaanza leo, lakini safari hii linadhihirisha jinsi wanavyo tapa tapa.
Kitisho cha AfD kugawika
Mada yetu ya mwisho magazetini inahusiana na mvutano ndani ya chama cha siasa kali za mrengo wa kulia "Chaguo Mbadala Kwa Ujerumani"-AfD na suala kama mwanachama wake mchokozi Björn Höcke afukuzwe chamani au la. Gazeti la "Südkurier" linaandika: "Ni nadra watu kukubaliana na hoja za kada wa AfD Gauland. Lakini katika kadhia hii, hajakosea. Mvutano kuhusu kufukuzwa chamani Björn Höcke unaweza kukigawa chama cha AfD. Mvutano huo umeripuka katika katika wakati ambapo AfD kilibidi kuwa kitu kimoja ili kuingia katika kampeni za uchaguzi mkuu. Badala yake wanahasimiana na hapatopita muda mrefu watatengana. Höcke anaweza kujinata kuwa shujaa wa AfD.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman