Tuvijue vilabu vya ligi kuu ya kabumbu nchini Ujerumani
20 Oktoba 2010Stadi wa dimba anaesababisha timu kupanda kileleni Felix Magath ana kabiliwa na kazi kubwa katika timu yake mpya ya FC Schalke 04.Alipokabidhiwa wadhifa wa kocha wa timu hiyo ya Gelsenkirchen mwaka mmoja uliopita,alijiwekea shabaha ya kutwaa taji la ubingwa mnamo muda wa miaka minne ijayo.Na alikua nusra akamilishe ndoto hiyo mnamo msimu wake wa mwanzo pamoja na Schalke 04 katika ligi kuu.Lakini hata yeye Magath anasumbuliwa na hali ngumu ya Schalke,
Hakuna timu yenye kiu kikubwa cha kutwaa taji la ligi kuu kama ile ya Schalke 04.Walitawazwa mabingwa kwa mara ya sabaa na ya mwisho miaka 52 iliyopita.Mara kadhaa walikuwa nusra wanyakue taji la ubingwa wa ligi kuu:Watoto wa Gelsenkirchen walikuwa makamo bingwa mara nne katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.Mwaka 2001 waliona uchungu kuliko mara zote nyengine:kwa muda wa dakika nne nzima,mnamo siku ya mwisho ya michauno ya ligi kuu, Schalke 04 walikua tayari wanajisikia kama mabingwa,kabla ya Bayern Munich katika pambano lake dhidi ya Hambourg SV,kujinyakulia pointi ilizokua ikizihitaji kutawazwa mabingwa.
Schalke wakazama katika bahari ya machozi na tangu wakati huo wamegeuka mabingwa wa nyonyo za mashabiki wao.Hata katika msimu uliopita,Schalke 04 walimaliza wapili,safari hiyo lakini ulikua ufanisi uliostahiki.Kocha Felix Magath aliwadhihirishia mashabiki wa soka sifa zake kama mtu mwenye kuzusha maajabu.Aliwateremsha uwanjani wanasoka vijana wasiojulikana mfano wa Lukas Schmitz,Christoph Moritz au Joel Matip na wakamshukuria kwa kuonyesha dimba maridadi kabisa.Magath hakuchelea lakini pia kupunguza matumizi pale alipoona ni lazma kufanya hivyo.Baada ya miaka kadhaa ya uzembe timu hiyo ilikuwa nusra ifilisike.
Kwa hivyo halikuwa jambo la kustaajabisha pale Felix Magath alipoamua kuachana na wachezaji wake waliokuwa wakiigharimu fedha nyingi timu hiyo, mfano wa Kevin Kuranyi anaechezea Moscow hivi sasa,Marcelo Bordon anaechezea Qatar,Heiko Westermann anaechezea timu ya Hambourg SV,na Gerald Asamoah anaeichezea FC St Pauli ya huko huko Hamburg pia.
BIla ya shaka kuna wachezaji wepya waliojiunga na Schalke mfano wa mchezaji nyota Raul aliyetokea Real Madrid.Mwengine ni Christopher Metzelder aliyeachana na Real Madrid na kurejea nyumbani katika eneo la mto Ruhr.Kocha Felix Magath anafurahia jambo hilo kinyume na mashabiki wa Schalke 04 na kusema:
"Christoph Metzelder mtu anaweza kumtaja kuwa mwanasoka anaeongoza.Nnaamini kwakua pamoja nae atasaidia kuipatia timu yetu sura ya dimba la kimataifa."
Mashabiki wangali bado wanaotea siku watakapotawazwa mabingwa,wakikumbuka taji la mwisho,mwaka 1997 Schalke 04 ilipotwaa kombe la UEFA na mwaka 2001 na 2002 kombe la shirikisho la kabumbu la Ujerumani-DFB
Mwandishi:Petersen,Uli/Hamidou Oummilkheir
Mpitiaji:M.Abdul-Rahman