1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UAE yapinga pendekezo la uchimbaji mafuta la OPEC

5 Julai 2021

Mawaziri wa nchi zinazosafirisha mafuta kwa wingi duniani, OPEC wanakutana kujadiliana tena kuhusu sera ya uchimbaji wa mafuta, baada ya kuvutana wiki iliyopita.

https://p.dw.com/p/3w3sS
Logo OPEC
Picha: Pavlo Gonchar/ZUMAPRESS.com/picture alliance

Mvutano huo ulisababishwa ha hatua ya Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE kulipinga vikali pendekezo la jumuia hiyo kuongeza kiwango cha uchimbaji wa mafuta kwa miezi minane. 

Waziri wa Nishati wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Suhail Mohamed Al-Mazrouei ameliambia shirika la habari la WAM kwamba umoja huo uko tayari kuongeza makubaliano ikiwa itahitajika kufanya hivyo, lakini inataka kupata kumbukumbu ya viwango vya mapato kuhakikisha viko sawa.

Mapipa ya mafuta yaliyosafirishwa

Oktoba mwaka 2018, Umoja wa Falme za Kiarabu ulisafirisha mapipa milioni 3.17 kwa siku, kikiwa ni chini ya kiwango cha ufanisi wa usafirishaji wa mapipa milioni 3.8 kwa mwezi Aprili mwaka 2020.

Akihojiwa na kituo cha televisheni cha Al-Arabiya jana usiku, Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Abdulaziz bin Salman ametoa wito wa kuwepo maelewano na busara itumike ili kufikia makubaliano, baada ya kushindwa kuafikiana kwa siku mbili katika mazungumzo ya wiki iliyopita.

''Juhudi kubwa zimefanywa katika kipindi cha miezi 14 iliyopita ambazo zilitoa matokeo mazuri na litakuwa jambo la aibu tukishindwa kudumisha mafanikio haya. Maelewano na busara ndiyo vitatuokoa,'' alifafanua Mwanamfalme Abdulaziz.

Saudi-Arabien -  Prinz Abdulaziz bin Salman
Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Abdulaziz bin SalmanPicha: Getty Images/AFP

Aidha, Mwanamfalme huyo amesema jumuiya nzima ya OPEC inavutana na Saudia ambayo imebaki peke yake, na kusisitiza kwamba jambo hilo linasikitisha sana.

Mwaka uliopita, OPEC ilikubaliana kupunguza pato la takribani mapipa milioni 10 kwa siku, kutokana na janga la virusi la corona. Kwa sasa jumuiya hiyo inasafirisha mapima yapatayo milioni 5.8 ya mafuta kwa siku.

UAE yasababisha mkwamo

Hatua ya Umoja wa Falme za Kiarabu kupinga pendekezo la OPEC imesababisha kizingiti kinachoweza kuzirudisha nyuma juhudi za kudhibiti kuongezeka kwa bei ya mafuta ghafi katika wakati ambapo kuna hali tete ya kujaribu kuukwamua uchumi kutokana na janga la COVID-19. Mkwamo huo unaweza ukachelewesha mipango ya kusafirisha mafuta zaidi hadi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, hatua inayoweza kuathiri bei ya mafuta duniani.

Soma zaidi: OPEC+ wakubaliana kushusha kiwango cha uzalishaji mafuta

Kulingana na duru, siku ya Ijumaa Umoja wa Falme za Kiarabu ulivutana na Saudi Arabia na wanachama wengine wa OPEC kuhusu pendekezo la kuongeza usafirishaji wa mafuta kwa takribani mapipa milioni mbili kwa siku kuanzia mwezi Agosti hadi Desemba mwaka huu.

Vyanzo viwili vya OPEC vimesema leo kwamba hakuna hatua iliyopigwa katika kulitafutia ufumbuzi suala hilo kabla ya kutano huo. Kwa mujibu wa duru hizo, OPEC inaweza kuendelea na mpango uliopo wa hadi Aprili, mwaka 2022 na kujadiliana kuhusu kiwango kipya cha Umoja wa Falme za Kiarabu kama sehemu ya mpango mpya.

(AFP, Reuters)