Uasi wa Wagner hautarejesha nyuma upatanishi wa Afrika
27 Juni 2023Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Afrika Kusini Naledi Pandor amewaambia waandishi habari kwamba ujumbe wa amani wa Afrika nchini Ukraine na Urusi utasonga mbele licha ya uasi wa Wagner.
Pandor aliyekuwa akizungumza mjini Pretoria akiwa na mgeni wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock, alisema ujumbe wa viongozi wa Kiafrika ulikuwa ni ziara ya awali nchini Urusi na Ukraine na kwamba viongozi wa mataifa hayo mawili walikubali kufanya mikutano zaidi katika wiki chache zijazo.
Soma zaidi: Baerbock kuzungumza na Pandor kuhusu Ukraine
Rais Cyril Ramaphosa na viongozi wengine wa Afrika walizitembelea Kyiv na Moscow mwezi huu kujaribu kutafuta suluhu ya mzozo unaoendelea.
Kwa upande wake, Baerbock, ambaye yuko ziarani nchini Afrika Kusini, amesema uasi uliozimwa nchini Urusi umeonesha Rais Vladimir Putin anaiharibu mwenyewe nchi yake.