1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ubalozi wa Marekani nchini Uturuki washambuliwa

20 Agosti 2018

Ubalozi wa Marekani nchini Uturuki, umeshambuliwa kwa risasi mapema hii leo, katika shambulizi ambalo limefanywa wakati kukizidi hali ya wasiwasi kati ya mataifa hayo mawili wanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

https://p.dw.com/p/33Qy2
Türkei US-Botschaft in Ankara
Picha: picture-alliance/NurPhoto/D. Cupolo

Hata hivyo hakukuripotiwa madhara yoyote na hakuna aliyedai kuhusika na shambulizi hilo, ambalo risasi tatu kati ya sita zilizofyatuliwa zilitua kwenye geti la ubalozi huo na dirisha lisilopenyesha risasi la chumba cha walinzi.

Msemaji wa ubalozi huo David Gainer ameelezea shukrani zake juu ya hatua za haraka zizilochukuliwa na jeshi la polisi la Uturuki baada ya shambulizi hilo la asubuhi, na kuthibitisha kuwa hakukuwa na ripoti ya majeruhi na kwamba wanalifanyia uchunguzi wa kina shambulizi hilo. Maafisa wa Uturuki ambao wameingia kwenye mgogoro wa kidiplomasia na Marekani, wamelaani tukio hilo lililotokea kwenye mji mkuu, Ankara. 

Msemaji wa chama tawala nchini humo cha Justice and Development, AKP, Omer Celik hii leo amesema shambulizi kwenye ubalozi wa Marekani lilikuwa na uchokozi dhahiri, huku akiyahahakikishia mataifa ya nje kwamba balozi zao ziko salama.

Alinukuliwa akisema "Kulingana na taarifa tulizonazo, kulifyatuliwa risasi sita. Tatu kati ya hizo zilipiga dirisha na tunashukuru Mungu hakukua na taarifa ya kifo ama majeruhi. Ni kweli, huu ni uchokozi dhahiri. Na kuna kazi nzito inafanyika kuhusu uchokozi huu. Eneo lile lina shughuli nyingi sana. Tukio lile lilitokea majira ya saa 11.30 alfajiri ya leo."

Türkei AKP Kongress in Ankara
Rais Recep Tayyip Erdogan amesema Uturuki haitayumbishwa na vitisho dhidi ya uchumi wake.Picha: picture-alliance/AA/K. Ozer

Lakini pia msemaji wa rais, Recep Tayyip Erdogan, Ibrahim Kalin aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter akisema lilikuwa ni jaribio lililolenga kusababisha machafuko.

Mvutano kati ya Marekani na Uturuki umeongezeka, kwa sehemu kwa sababu ya kesi ya mchungaji wa Kimarekani, Andrew Brunson, anayetuhumiwa na Uturuki kwa ujasusi na makosa yanayohusiana na ugaidi, ambayo mchungaji huyo anayakana. Rais Donald Trump wa Marekani alitaka kuachiwa mara moja kwa mchungaji huo.

Mapema, rais Erdogan, ambaye serikali yake pia imeweka ushuru wake kwenye baadhi ya bidhaa za Marekani, ameuzungumzia mzozo baina yao, katika ujumbe wa sikukuu uliorekodiwa. Alisema shambulizi dhidi ya uchumi wa Uturuki, haliwezi kutofautishwa na shambulizi dhidi ya mwito wa sala ama adhana na bendera yao, kwa kuwa yote yanalenga kuididimiza Uturuki na watu wake na kuwafanya mateka.

Rais Erdogan alisema "Wale wanaodhani wanaweza kuishinikiza  Uturuki kwa viwango vya kubadilisha fedha, wale waliojaribu awali pamoja na makundi ya kigaidi  na mitandao ya wasaliti wa ndani , karibuni watajiona kuwa wamekosea. Kwa nguvu ya Allah, Uturuki ina nguvu na uwezo wa kukabiliana na mzozo, ali mradi tu tunakuwa  pamoja."

Hivi karibuni Marekani iliiwekea vikwazo vya kiuchumi Uturuki, ikiwa ni pamoja na ushuru wa bidhaa ya chuma cha pua na bati, hatua iliyochangia kuanguka kwa thamani ya sarafu ya Uturuki ya Lira.

Mwandishi: Lilian Mtono/APE/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman