Uchaguzi Guinea
3 Desemba 2010Alpha Conde amechaguliwa kuwa rais mpya nchini Guinea. Mahakama kuu nchini humo imethibitisha matokeo ya uchaguzi wa kwanza huru uliofanyika nchini humo tangu Guinea ijinyakulie uhuru, na ambao ulikumbwa na vita vya kikabila.
Baada ya kusubiri kwa muda wa wiki mbili chini ya hali ya hatari iliyotangazwa kufuatia kuzuka kwa vurugu baada ya matokeo ya kwanza ya uchaguzi huo kudhihirisha Alpha Conde anaongoza kwa wingi wa kura, mahakama kuu ya Guinea hii leo imethibitisha ushindi wake wa asilimia 52.52.
Hakimu Mamadou Sylla wa mahakama hiyo anayesimamia idara ya sheria, aliwaambia waandishi wa habari kwamba mgombea huyo wa chama cha RPG ndiye aliyeibuka mshindi.
Mpinzani wake Cellou Dalein Diallo ambaye wafuasi wake walimiminika barabarani wakilalamika kwamba uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu, alijinyakulia asilimia 47.48 ya kura hizo.
Mapema leo asubuhi, hali ilikuwa shwari nchini humo baada ya mahakama hiyo kuu kutoa tangazo hilo. Mamia ya wafuasi wa Conde walionekana wakisherehekea nje ya makaazi yake lakini kiongozi huyo mpya hakutaka kuhojiwa na waandishi wa habari.
Mahakama hiyo ilikataa kupokea ombi la Diallo,aliyetaka matokeo ya maeneo mawili, ya Siguiri na Kouroussa yafutiliwe mbali.
Diallo alilalama kwamba kabila la Malinke linalo muunga mkono Conde, lilizusha chuki za kikabila dhidi ya kundi lake la kabila la Fulani, katika maeneo hayo mnamo mwezi wa Oktoba.
Vurugu zilizozuka baada ya kutolewa kwa matokeo ya muda tarehe 15 mwezi uliopita, zilisababisha vifo vya watu takriban 7 na mamia kujeruhiwa, huku maafisa wa usalama wakifanya misako kufuatia shutuma za kimataifa dhidi ya mauaji yasiyohitajika.
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch, limesema vikosi vya usalama vilivyo na idadi kubwa ya watu wa kabila linalomuunga mkono Conde, vilitumia nguvu ya kupita kiasi dhidi ya watu wa kabila la Fulani.
Hapo jana wagombea wote wawili walitoa wito wa kudumishwa amani katika mahojiano waliofanyiwa kila mmoja upande wake, kwenye vituo vya redio.
Conde aliahidi akichaguliwa, atakuwa rais wa raia wote nchini humo kwa kuwaleta pamoja na kudumisha suluhu.
Hii ni mara ya tatu kwa Conde kuwania kiti hicho cha rais na ameshinda katika uchaguzi huo uliopongezwa kuwa huru na wa kidemokrasia tangu nchi hiyo ijinyakulie uhuru kutoka kwa Ufaransa mnamo mwaka 1958 baada ya utawala wa kidikteta na wa kijeshi .
Guinea ambayo ni nchi maskini licha ya kuwa na utajiri wa madini, imekuwa katika mzozo wa kisiasa tangu jaribio la mapinduzi mwezi Desemba mwaka 2008 lililofuatwa na kifo cha kiongozi wa kijeshi wa muda mrefu, Lansana Conte.
Mwandishi Maryam, Abdalla/AFPE
Mpitiaji:Hamidou Oummilkheir