1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi Misri

MjahidA26 Mei 2012

Mohammed Mursi na Ahmed Shafiq kupambana katika duru ya pili ya uchaguzi Misri

https://p.dw.com/p/152n1
Mgombea wa Urais wa chama cha Muslim Brotherhood nchini Misri Mohammed Mursi
Mgombea wa Urais wa chama cha Muslim Brotherhood nchini Misri Mohammed MursiPicha: AP

Mgombea  Urais wa chama cha Muslim Brotherhood Mohammed Mursi na  Ahmed  Shafiq, aliekuwa Waziri mkuu  katika utawala wa Hosni Mubarak watapambana katika raundi ya pili ya uchaguzi nchini Misri.

Hii ni kwa mujibu  wa matokeo ya raundi ya kwanza ya uchaguzi ambayo siyo rasmi yanayoendelea kutolewa nchini humo. Raundi ya pili ya uchaguzi imepangwa  kufanyika tarehe 16 hadi 17 mwezi ujao.

Chama cha Muslim Brotherhood kinajaribu kuungana na wanasiasa wengine wanaomuunga mkono Mursi ili amshinde Shafiq anaezingatiwa kuwa  mtu aliyetoka katika utawala wa Mubarak na tishio kwa mapinduzi  yaliyomwondoa  Mubarak madarakani.

Mgombea wa urais Ahmed Shafiq, aliyekuwa waziri mkuu Misri
Mgombea wa urais Ahmed Shafiq, aliyekuwa waziri mkuu MisriPicha: AP

Katika mahojiano na shirika la televisheni la kibinafsi  Shafiq alisema haoni tatizo iwapo waziri mkuu atatoka katika chama cha Freedom and Justice.

Kwa  mujibu  wa matokeo ambayo siyo rasmi Mgombea wa chama cha Muslim Brotherhood Mohamed Mursi aliwashinda wagombea wengine katika duru ya kwanza ya uchaguzi.

Hata hivyo matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa jumanne ijayo. Raundi ya pili ya uchaguzi itakuwa muhimu sana kwa watu wa Misri na kwa eneo lote linalopakana Misri.

Raundi ya pili itawapa wapiga kura fursa ya kuchagua  kuendelea kuongozwa na mtu anaetokea jeshini au kuichagua serikali itakayoongozwa na mtu anaetokea katika kundi lililokandamizwa kwa muda mrefu lakini lenye ushawishi mkubwa katika eneo linalopakana na Misri.           

Itakumbukwa kwamba Mohammed alisema katika kampeni zake mateso waliyokuwa wakiyapata Wamisri chini ya utawala wa Hosni Mubarak ni kwa ajili ya sheria za Kiislam na kwamba damu yao na kuishi kwao kunategemea utekelezaji wa azma hiyo, na kuongeza kuwa kwa pamoja watapigana kutekeleza azma hiyo.

Asili mia 50 ya wapiga kura wameshiriki uchaguzi wa sasa wa urais nchini Misri.

Mwandishi Amina Abubakar/AFP/Reuters

Mhariri Abdu-Mtullya