1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi mkuu wa Liberia wafanyika leo

11 Oktoba 2011

Wapiga kura milioni 1.8 wa Liberia wanateremka vituoni kuwachagua rais, wabunge na maseneta katika uchaguzi unaoangaliwa kama muhimu katika kuimarisha amani, miaka 8 baada ya kumalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe .

https://p.dw.com/p/12q1w
Rais anaemaliza wadhifa wake Ellen Johnson-SirleafPicha: DW

Rais anaemaliza wadhifa wake, Ellen Johnson Sirleaf, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel kwa mwaka huu wa 2011, atashindana na wagombea 15, akiwemo mkuu wa chama cha upinzani cha Kongamano la Mageuzi ya kidemokrasi-CDC- Winston Tubman, anaeteremka kwa tikiti moja pamoja na mchezaji nyota wa zamani wa soka-George Weah.

Ellen Johnson Sirleaf anawania mhula wa pili madarakani kwa hoja kwamba lengo lake la kuimarisha utulivu nchini Liberia baada ya vita vya miaka 14 bado halijakamilika.

"Uchaguzi wa leo umelengwa kupima moyo wa waliberia katika kusimamia wenyewe chaguzi zao na kuhakikisha zinapita kwa njia huru na ya haki" amesema hayo mkuu wa tume ya uchaguzi-NEC,James Fromayan.

Winston Tubman Liberia Präsidentschaftskandidat
Winston Tubman wa kutoka chama cha upinzani cha CDCPicha: picture alliance/dpa

Wasimamizi zaidi ya elfu tano ,wakiwemo 800 wa kimataifa, wanasimamia uchaguzi huo.

Muda mrefu kabla ya vituo kufunguliwa, mililolongo ya watu walipiga foleni mbele ya vituo vya upigaji kura licha ya manyunyu ya mvua iliyokuwa ikinyesha katika mji mkuu, Monrovia.

"Ninafurahi kuweza kupiga kura. Ni uchaguzi muhimu kwa utulivu wa kiuchumi na neema nchini Liberia na ndio maana nimekuja mapema sana", amesema mpigaji mkura mmoja mwenye umri wa miaka 37 alipohojiwa na shirika la habari la Ufaransa, AFP.

Kwa mujibu wa kituo cha usimamizi cha rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter, ambacho kimetuma wataalam 40 katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi, matokeo ya awali yanatarajiwa kutangazwa saa 48 baada ya viituo vya upigaji kura kufungwa.

Mshindi mwenza wa tuzo ya amani ya Nobel, aliyechaguliwa mwaka 2005 kushika hatamu za uongozi, akiwa rais wa kwanza wa kike barani Afrika, amekuwa akilaumiwa sana na Winston Tubman ambae kabla ya uchaguzi alikuwa mshirika wale mkubwa.

Wahlen in Liberia
Vijana wanategemea mengi kutokana na uchaguzi huuPicha: DW

Ingawa bibi Ellen Johnson-Sirleaf anajivunia sifa katika jumuia ya kimataifa, nyumbani, lakini, kuna wengi wanaomkosoa. Wanamsuta kwa kuahidi mwaka 2005 kugombea mhula mmoja tu. Wengi wanakosoa ukosefu wa uwazi katika serikali yake.

Ben Saly ni miongoni mwa waliompigia kura bibi Johnson Sirleaf uchaguzi wa kwanza wa baada ya vita ulipoitishwa mnamo mwaka 2005. Hii leo kijana huyo ambae hana kazi analalamika na kusema tunanukuu: "Ni shida kwetu kupata kazi na mpaka leo bado kuna ukosefu wa umeme katika maeneo tofauti", mwisho wa kumnukuu kijana huyo anaemalizia kwa kusema safari hii hatompigia kura rais huyo anaemaliza wadhifa wake.

Duru ya pili ya uchaguzi itafanyika November nane ijayo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir(dpa/afp)

Mhariri:Miraji Othman