Uchaguzi mkuu wa Ujerumani magazetini
23 Septemba 2013Mada mja tu ndio iliyohodhi vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani:Ushindi wa kansela Angela Merkel na chama chake cha CDU katika uchaguzi mkuu.
Tuanzie na gazeti la "Reutlinger General-Anzeiger" linalosema hii ni jaza kwa kansela Angela Merkel."Gazeti linaendelea kuandika:"Kansela amejipatia ushindi ambao vyama ndugu vya CDU/CSU havijawahi kujivunia kwa takriban miaka 20 iliyopita.Wataalam wa masuala ya kisiasa walikuwa tayari wanaashiria mwisho wa enzi za vyama vikuu -Angela Merkel lakini amedhihirisha kinyume chake.Tayari imeshabainika kwanini katika kampeni za uchaguzi,visa kama vile vya Steinbrück kuonyesha kidole cha kati au "siku ya chakula cha mboga mboga" ya walinzi wa mazingira vimegonga zaidi vichwa vya habari kuliko mijadala kuhusu ratiba za uchaguzi.CDU,Angela Merkel anawatosha.Lakini wakati huo huo na katika historia ya shirikisho la jamhuri ya Ujerumani,chama cha FDP hakiwakilishwi tena katika bunge la shirikisho-Bundestag.Pigo kubwa hilo ambalo sababu zake ni nyingi ikiwa ni pamoja pengine na mabadiliko katika mfumo wa vyama vya kisiasa humu nchini.
FDP nje ya medani ya kisiasa
Gazeti la mjini Berlin "Berliner Zeitung" linamulika hali iliyopelekea FDP kupigwa kumbo.Gazeti linaendelea kuandika:"Ukweli kwamba FDP hawatowakilishwa tena katika bunge la shirikisho-Bundestag na kwamba wamepigwa kumbo katika takriban mabunge yote ya majimbo ni pigo kubwa.Lakini ni pigo ambalo chama hicho cha kiliberali kimejitakia wenyewe kutokana na mivutano ya mara kwa mara ya viongozi wa chama hicho.Mivutano ya kuania uongozi na sera za kuania masilahi ya makundi maalum ndio chanzo kilichokifanya chama hicho kupoteza mizizi yake ya kiliberali.Chama kinachodai kinataka kutawala lakini bila ya kutamka kwanini hakistahiki tena kuchaguliwa."
Gazeti la "Flensburger Tageblatt linahofia ushindi mkubwa wa kansela usije ukamtumbukia nyongo".Gazeti linaendelea kuandika:"Kansela Angela Merkel amekipatia chama cha CDU ushindi mkubwa.Kampeni ziliendeshwa kama zilimlenga yeye.Lakini ushindi wake unaweza kuwa mzigo kwa vyama ndugu vya CDU/CSU.Mshirika waliekuwa nae hadi sasa ametoweka.Msimamo wake wa wastani unaoelekea mrengo wa kati na SPD,umempatia matatizo kutoka kwa wafuasi wa mrengo wa kulia wa CDU/CSU.Baadhi ya wahafidhina wanakiangalia chama cha Chaguo Mbadala-AfD kama mtihani kwa CDU.
Na SPD wanaelekea wapi?
Nalo gazeti la "Kieler Nachrichten linakimulika chama cha SPD na kuandika:"Baada ya maafa yanafuatia machungu.Baada ya matokeo ya pili mabaya kushuhudiwa katika uchaguzi mkuu,chama cha SPD hakiwezi kushiriki serikalini na kuwaacha viongozi wake kama walivyo.Pengine hali itakuwa nyengine .Pengine SPD na viongozi wake watatu watazungumza na CDU/CSU kuunda serikali.Lakini kama hilo ndilo litakalokiokoa chama cha SPD-kuna wanaobisha.Katika serikali ya kwanza ya muungano wa vyama vikuu iliyoongozwa na Angela Merkel,SPD walikuwa na nguvu takriban sawa na CDU/CSU.Safari hii lakini hali ni tofauti.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlnadspresse
Mhariri:Yusuf Saumu