Uchaguzi mkuu waanza Nigeria
7 Aprili 2011Waangalizi wa Umoja wa Ulaya pamoja na wa Afrika tayari wamewasili nchini humo kuhakikisha kuwa mazingira ya uchaguzi huo yanavitimiza vigezo vya uhuru na haki.Zoezi hilo litafikia kilele chake tarehe 9 atakapochaguliwa rais mpya wa Nigeria.
Wiki tatu
Uchaguzi huo wa wabunge,rais na serikali za mitaa unaanza rasmi hii leo (02.04.2011) na utaendelea hadi tarehe 16 mwezi huu.Kilele chake ni uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika tarehe 9.Rais aliye madarakani Goodluck Jonathan wa chama tawala cha People's Democratik, atapambana na Makamu wake Namadi Sambo anayeiwania pia nafasi hiyo.Kinyang'anyiro hicho kinaaminika kitakuwa na ushindani mkubwa kwani vyama vitatu vikuu viwasilisha wagombea wao ambao wanatokea eneo la kaskazini la Nigeria lililo na waislamu wengi.Kulingana na afisa mmoja wa serikali,zoezi la kuwasajili wapiga kura lilihitimishwa bila matatizo yoyote makubwa na mfumo mpya uliotumiwa utayatimiza malengo yake.Damieari von Kennedy anaelezea kuwa , "Daftari la wapiga kura linaaminika kwasababu mfumo uliotumiwa kuwasajili wapiga kura ni wa teknolojia ya hali ya juu na wanaweza kuzuwia uwezekano wa kuwasajili watu mara mbili mbili.Ninaamini kuwa Tume ya uchaguzi ya IINEC ilifanya kazi nzuri.
Milioni 73 wamesajiliwa
Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya wapiga kura milioni 73 wamesajiliwa ili washiriki katika uchaguzi. Suala la usalama limejitokeza hivi karibuni kufuatia visa vya ghasia vilivyosambaa wiki chache kabla ya uchaguzi huu kuanza.Kwa mujibu wa Kamishna wa Kitaifa wa Tume ya Uchaguzi ya Nigeria, INEC , Adedeji Soyebi aliyezungumza na shirika la habari la Reuters,kila kibanda cha kupigia kura kitalindwa na kikosi maalum cha usalama.Wajibu wa wanajeshi ni kupiga doria kuhakikisha usalama unadumishwa mitaani.
Uhuru,haki pasina Vitisho
Wakati huo huo ,waangalizi wa Umoja wa Ulaya na Afrika tayari wameshawasili nchini humo.Katika taarifa yao ya pamoja,Taasisi ya masuala ya demokrasia,Shirika la waangalizi wa Jumuiya ya Madola-Commonwealth,Ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Ulaya na Taasisi ya kimataifa ya Republik wamekiri kuwa raia wa Nigeria wanataka kushiriki kwenye zoezi ambalo litakuwa huru,haki na bila ya vitisho.
Kiasi ya wagombea 7 wanawania wadhifa wa urais katika uchaguzi huu ambao ni wa tatu kufanyika tangu Nigeria irejee kwenye mfumo wa demokrasia mwaka 1999.Rais Jonathan Goodluck ambaye ni Mkristo anayetokea eneo la kusini la Bonde la Niger anachuana na kiongozi wa kijeshi wa zamani Muhammadu Buhari ambaye ni Muislamu aliyeng'olewa madarakani baada ya kuongoza kwa miaka miwili pekee.Buhari aliingia madarakani mwaka 1983.
Ushindani: Wagombea wa nguvu
Wagombea wengine ni mkuu wa zamani wa shirika la kupambana na ufisadi Nuhu Ribadu wa chama cha Action Congress ana wafuasi wengi baadhi ya maeneo ya kusini magharibi. Ibrahim Shekarau ambaye ni gavana wa jimbo la Kano lililo eneo la kaskazini naye pia anawania wadhifa huo.
Kulingana na utaratibu wa uchaguzi,mshindi wa uchaguzi wa urais sharti apate wingi wa kura na kiasi ya asilimia 25 ya kura zote katika thuluthi mbili ya majimbo yote 36 ya nchi. Matokeo ya aina hiyo yanamhakikishia mgombea ushindi katika duru ya kwanza.
PDP kiko ngangari
Ifahamike kuwa chama tawala cha PDP kimefanikiwa kuibuka washindi katika kila uchaguzi wa rais tangu utawala wa kijeshi kumalizika mwaka 1999.Kwa sasa kina zaidi ya robo tatu ya viti vyote bungeni na kinawakilishwa katika majimbo 27 kati ya yote 36 nchini Nigeria.Hata hivyo upinzani una imani kuwa juhudi zao za kikanda zitachangia katika ushindi wao.
Mwandishi:Mwadzaya,Thelma-RTRE/AFPE
Mhariri: Hamidou Oummilkheir