1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi nchini Ujerumani 2009

Sekione Kitojo26 Septemba 2009

Chama cha kansela Angela Merkel cha Christian Democratic Union CDU , kinaelekea kupata ushindi kwa mujibu wa maoni ya wapiga kura.

https://p.dw.com/p/JpPk
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, kushoto, na waziri wa fedha Peer Steinbrueck, kulia wakijadiliana jambo, Septemba September , 8, 2009 bungeni mjini Berlin.Picha: AP

Vyama vya kisiasa vilikuwa vinafanya juhudi za mwisho jana Ijumaa kuwashawishi wapigakura ambao bado hawajaamua watapiga kura zao kwa chama gani , kuwapigia kura katika uchaguzi utakaofanyika kesho Jumapili hapa nchini Ujerumani, ambapo ushindi kwa kansela Angela Merkel unaonekana ni hakika.

Maoni ya wapiga kura yanatabiri kuwa chama cha kansela Angela Merkel cha Christian Democratic Union CDU kitapata sehemu kubwa ya kura na kufanikiwa kupata ushindi kwa kupata kuungwa mkono vya kutosha na kukitupilia mbali chama cha Social Democratic SPD na kuunda serikali mpya na chama kinachopendelea wafanyabiashara cha Free Democratic FDP.

Matthias Jung anayechukua maoni ya wapiga kura ametabiri ushindi mwembamba, lakini wa uhakika wa kupata wingi kwa muungano wa vyama vya nyeusi na njano, akimaanisha rangi za vyama vya CDU na FDP.

Anayegombea kiti cha ukansela pamoja na Merkel, waziri wa mambo ya kigeni Frank-Walter Steinmeier, amewahimiza waungaji wake mkono kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura wakati alipohutubia mkutano wa hadhara jana jioni katika eneo maarufu la mjini Berlin la lango la Brandenburg.

Steinmeier amesema muungano kati ya CDU na FDP utaigawa Ujerumani. Tunapaswa kupambana kuzuwia hali hii, amesema Steinmeier. Nani anataka kuuona muungano wa nyeusi na njano ukitawala nchi yetu ? Ni mabenki na makampuni ya bima.

Ujerumani ina matumaini makubwa ya hapo baadaye. Hali hii ya baadaye iko mikononi mwetu, amesema kiongozi huyo, ambaye chama chake cha SPD kiko nyuma ya chama cha kansela Merkel katika maoni ya wapiga kura.

Muungano wa CDU, FDP unaweza kutaraji kupata ushindi wa asilimia 48 hadi 48.9 ya kura, kwa mujibu wa kundi la utafiti wa maoni ya wapiga kura la Forsa na Allensbach, ikiviweka vyama hivyo asilimia moja hadi mbili mbele ya kura za jumla za kundi la vyama vya mrengo wa shoto, yaani SPD, chama cha kijani , Greens na chama cha mrengo wa shoto cha Die Linke.

Wakati chama cha SPD hakiondoi uwezekano wa kuingia katika serikali na chama cha mrengo wa shoto cha Die Linke, chama cha CDU na FDP haviwezi kuunda muungano imara bila ya kupata wingi wa kutosha katika bunge.

Njia mbadala kwa serikali ya muungano kati ya CDU na FDP kwa hiyo inaweza kuwa kurejewa tena kwa kile kinachoitwa muungano mkuu kati ya CDU na SPD.

Jung mkuu wa kundi la utafiti wa maoni ya wapiga kura , ametabiri kuwa SPD itapata asilimia ya chini ya 25 asilimia, ikiwa hata hivyo ni kiwango bora kutokana na utabiri uliopita lakini hata hivyo ni ndogo mno kuliko kiwango kinachotabiriwa CDU kupata cha asilimia 35 hadi 36.

Katika hatua za mwisho za kampeni, Merkel ameonekana akipeana mkono na rais wa Marekani Barack Obama katika mkutano wa kundi la mataifa ya G20, kuliko kuzungumza katika mikutano wa hadhara nchini Ujerumani.

Akionyesha nafasi yake kama kiongozi wa nchi , Merkel amejitokeza katika medani ya dunia mjini Pittsburg, katika jimbo la Pennsylvania, akifuatana na waziri wa fedha Peer Steinbrueck kutoka chama cha SPD, katika kile kinachoonekana kuwa ni mara ya mwisho watu hao kujitokeza kwa pamoja.

Wanasiasa hao wote wawili wanafaidika na muungano wao katika mkutano huo unaojaribu kutatua mzozo wa kiuchumi, Merkel akionyesha uwezo wake wa kujitokeza mbali na siasa za kichama, wakati Steinbrueck ameweza kuimarisha hali ya chama chake cha SPD kuaminika kuwa mshirika sahihi wa serikali.

Uchumi unajenga kiini cha kampeni za uchaguzi, wakati vyama vimekuwa vikijaribu kutoa ufumbuzi wa mzozo huo, unaonekana na baadhi ya watu kuwa ni kiwingu kinachofunika matatizo makubwa zaidi ya ndani, kama sera zinazohusu idadi kubwa ya watu nchini Ujerumani ambao ni wazee.

Wimbi la video za kundi la kigaidi la al-Qaeda katika muda wa wiki moja iliyopita zimekuwa zikiwatishia Wajerumani kutokea milipuko nchini humo iwapo wapiga kura wataunga mkono serikali ambayo inaunga mkono vita nchini Afghanistan, ambapo wanajeshi 4,200 wa Ujerumani wanashiriki katika jeshi la kimataifa nchini humo.

Mwandishi Sekione Kitojo / RTRE

Mhariri Prema Martin.