1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa bunge nchini Serbia

Hamidou, Oumilkher12 Mei 2008

Chama cha rais Boris Tadic kinaonyesha kujikingia wingi wa kura

https://p.dw.com/p/DyOe
Rais Boris Tadic akishanagiriwa matokeo ya uchaguzi yalipotangazwaPicha: AP


Chama cha rais Boris Tadic, kinachoelemea upande wa Umoja wa Ulaya nchini Serbia,kimeibuka na ushindi bila ya kutarajia,kufuatia uchaguzi wa bunge uliotishwa kabla ya wakati.Idadi ndogo ya wapiga kura walioteremka vituoni iliwafanya wadadisi waamini pengine wafuasi wa kizalendo wangeshinda.


 Hata hivyo ushindi huo hautoshi kuweza kupitisha maamuzi muhimu bungeni.Kwa mujibu wa makadirio yaliyotangazwa hadi sasa, chama kinachoongozwa na rais Boris Tadic,na washirika wake,wamejikingia asili mia 38.7 ya kura dhidi ya asili mia 29.1walizojipatia wafuasi wa chama cha siasa kali za kizalendo kinachoongozwa na Tomislav Nikolic,huku chama cha waziri mkuu Vojislav Kostunica kimekamata nafasi ya tatu kwa asili mia 11 ya kura.


Umoja wa ulaya umesifu matokeo hayo.

Uchaguzi huo wa bunge ulioitishwa kabla ya wakati ulifungamanishwa na suala kama waserbia wanapendelea au la kuujongelea Umoja wa ulaya-lengo alilojiwekea rais Tadic-kabla ya uchungu uliosababishwa na uamuzi wa waKosovo kujitangazia uhuru wao,wakiungwa mkono na baadhi ya nchi za umoja huo.


Akihutubia mbele ya wafuasi wa chama chake waliojaa furaha,mjini Belgrade,rais Boris Tadic amesema:


"Wananchi wa Serbia wameunga mkono kujiunga nchi yao na Umoja wa ulaya.Serikali tutakayoiunda hivi sasa,haitautambua kwa namna yoyote ile uhuru wa Kosovo."


Katika wakati ambapo fash fash na muziki umehanikiza katika mji mkuu wa Serbia-Belgrade,mkuu wa upande wa upinzani,Tomislav Nikolic anabisha matokeo ya uchaguzi huo akisema kuna uwezekano mkubwa wa kuundwa serikali ya muungano bila ya kukijumuisha chama cha Democratic cha rais Tadic.


Amemtuhumu rais Tadic kwenda kinyume na muongozo wa katiba kwa kutaka kukitenga chama chake cha siasa kali za kizalendo.Kiongozi huyo wa chama cha asiasa kali za kizalendo amesema tunanukuu:


"Uchaguzi umedhihirisha lengo kubwa la waserbia walio wengi ni kulinda mamlaka yao katika mipaka inayotambulika kimataifa na suala la kujiunga na Umoja wa Ulaya linakuja nafasi ya pili tuu."Mwisho wa kumnukuu Tomislav Nikolic.


Wafuasi wa siasa kali wanaweza kuungana na chama cha kijamaa cha kiongozi wa zamani wa Serbia,Slobodan Milosovic na  kile cha waziri mkuu anaemaliza wadhifa wake,mhafidhina Vojislav Kostunica.


Kostunica,ambae umashuhuri wake umeshaanza kufifia amekwepa kuashiria aina yoyote ya muungano.Hata hivyo wakati wa mkutano pamoja na waandishi habari amezungumzia juu ya "hitilafu za maoni zisizosawazika pamoja na Tadic."





►◄