Uchaguzi wa CHADEMA wazusha maswali uwakilishi wa wanawake
23 Januari 2025Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema ukosefu wa kanuni na miongozi kwenye katiba za vyama vya siasa ndicho chanzo cha mapengo hayo ya kijinsia.
Mwenyekiti mpya wa CHADEMA, Tundu Lissu, amekamilisha uteuzi wa safu ya juu ya viongozina kuwapendekeza mbele ya Baraza Kuu, John Mnyika kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Amani Golugwa kuwa Naibu Katibu Mkuu - Bara huku upande wa Zanzibar, akimpendekeza Ali ibrahimu Juma. Uteuzi huu unafanya uongozi wa juu wa chama hicho kushikiliwa na wanaume tu, jambo ambalo wachambuzi wa masuala ya siasa na uongozi wameonyesha wasiwasi wao hasa kuhusu ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi ndani ya chama hicho.
Dk Consolatha Surey, Mhadhiri wa Shule ya Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema kukosekana kwa kanuni zinazokitaka chama kuweka usawa wa uongozi kwa kuzingatia jinsia, ndicho chanzo cha pengo hilo ndani ya CHADEMA.
“Kama hakutakuwa na nia Madhubuti kwamba sisi ndani ya chama chetu tunataka kuhakikisha kwmaba, tunayajumuisha haya makundi yaliyoachwa nyuma, kama hakuna hizo kanuni mahsusi, huyu Mwenyekiti halazimishwi kuzingatia hizo tofauti zilizopo, na hiyo sio shida ya CHADEMA, ni shida ya nchi yetu vile vile”
Soma pia: Lissu ambwaga Mbowe uenyekiti CHADEMA
Hata hivyo, Lissu kwa kutumia mamlaka yake kikatiba aliwachagua wajumbe wa kamati kuu ya CHADEMA na kuwateua Rose Mayemba na Godbless Lema. Dk Consolatha Surey amesema ukosefu wa ushiriki wa wanawake katika nafasi za juu za uongozi si kwa CHADEMA pekee bali hata katika vyama vingine vya siasa bado kuna changamoto.
Hata hivyo aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche amesema, watanzania wawe na Subira, bado teuzi ni nyingi ndani ya chama hicho.
“Unajua kwamba lazima akinamama wapewe nafasi na wapewe nguvu za uongozi, na tunafanya hivyo, na ndio maana katika teuzi za mwanzo kabisa, Mheshimiwa Lisu ameteua wanawake wawili kuwa wajumbe wa kamati kuu ya chama, ambao ‘actualy’ ndio ‘governing body’ ndio waamuzi”
Kwa upande wake, Mwanaharakati wa masuala ya jinsia na Mkurugenzi wa Kituo cha Sauti Kipunguni, Selemani Bishagazi amesema, changamoto ipo kwa wanawake wenyewe ndani ya vyama vya siasa.
“Hawajitokezi sana kuwania hizo nafasi za juu, wamewekeza sana kwenye ubunge na udiwani, kwenye chama huku wanajua kuna sekeseke la michango sekeseke la nini”
Chadema juzi ilikamilisha uchaguzi wake na kumpata Mwenyekiti mpya wa CHAMA hicho, Tundu Lissu, ambaye anakwenda kukiongoza chama kwa miaka mitano ijayo. Lissu anamrithi Freeman Mbowe, ambaye amekuwa kiongozi wa chama hicho kwa miongo miwili.