Uchaguzi wa Gabon wanukia
27 Agosti 2009Wananchi wa Gabon,nchi yenye utajiri wa mafuta wanasubiri kwa hamu kupiga kura katika uchaguzi wa rais siku ya jumapili.Mwanawe marehemu rais Omar Bongo,Ali Bongo pia ni mmoja wa wagombea wa Urais akitoa ahadi za kuboresha maisha kwa wananchi wa taifa hilo.
Hata hivyo wanasiasa wengi wa upinzani wanasema kwamba matokeo ya uchaguzi huo yameshapangwa hata kabla ya zoezi la kupiga kura na kwamba Ali Bongo ameshahakikishiwa kurithi madaraka.
Gabon ni nchi iliyojaaliwa utajiri mkubwa wa mafuta,ni nchi ya nne ya kusini mwa jangwa la sahara inayotoa mafuta kwa wingi na juu ya hilo ni nchi ya tatu duniani inayotoa madini ya manganese kwa wingi na pia ni nchi ya pili barani Afrika inayosafirisha mbao.Pamoja na utajiri huo wote lakini umaskini na rushwa ndio matatizo makubwa yanayowakabili wananchi wake.Inakadiriwa kwamba asilimia 60 ya idadi ya watu millioni 1.5 wanaishi chini ya kiwango cha umaskini. Barabara nyingi nchini humo zimeharibika kiasi cha kutotambulika kama ilivyo sekta ya afya na mifumo ya elimu ambazo zimesambaratika kabisa.Matatizo yote hayo yamejitikeza kutokana na ukweli kwamba akiba ya mafuta ya nchi hiyo imeanza kumalizika.
Wananchi wengi wa Gabon kwa hivyo wanasubiri kwa hamu kuona uchaguzi huo wa kwanza tangu kifo cha rais wake mnamo mwezi Juni.Wananchi wanasubiri kuona ikwa utajiri wa nchi hiyo utawafikia hata watu wasiokuwa kutoka familia ya Bongo pamoja na mtandao wa washika wao na vyama vyao.
Casimir Oye Mba mmoja wa wagombea 23 wa urais na ambaye ni waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo amesema kwamba ni asilimia 2 pekee ya idadi ya watu wa nchi hiyo ndio wanaofaidika na utajiri wa taifa hilo hali ambayo inabidi ibadilike msimamo ambao pia unaungwa mkono na mgombea mwengine wa Urais Pierre Mamboundou.
Ali Bongo mwanawe marehemu rais Omar Bongo anaangaliwa kama mtu atakayeshinda katika uchaguzi huo ingawa wagombea wengine 12 wametoa mwito uchaguzi huo uhairishwe kwasababu ya kile walichokitaja kuwa dosari za dhahiri ambazo zimeshajitokeza kabla ya uchaguzi.
Wagombea ambao ni wapinzani wa karibu wa Ali Bongo ni Oye Mba na Pierre Mamboundou na wote wanaungwa mkono na chama tawala cha GDP Gabonese Demokratic Party na hata vyombo vya kampeini.Hata hivyo kukosekana kwa vyombo vya kutoa kura za maoni za kuaminika ni suala linalochangia kuzusha wasiwasi kuelekea matokeo ya uchaguzi.
Mchambuzi mmoja wa masuala ya kisiasa kutoka mjini Libreville ambaye hakutaka kujitaja jina amesema kwamba ni wazi kwamba Ali Bongo atashinda uchaguzi ndiye anayependelewa.Chama tawala cha GDP kimezoea kudhibiti chaguzi zote nchini humo na mtu anaweza kuchaguliwa na hata chini ya asilimia 20 ya kura kwasababu kuna wagombea wengi sana.Fridolin Mve Messa,katibu mkuu wa chama cha waalimu yeye anasema
''Watu wamekuwa wakakamavu na yaliyojitoza katika mwaka wa 1993 huenda yakajirudia kwasababu uuma ulijitokeza kutetea kura zao lakini kwa kujitoza jeshi juhudi zao zilizuiwa.Kwa hiyo mwaka huu watu wako tayari kutetea uamuzi wao''
Hata hiyvo hasira za wananchi dhidi ya familia ya Bongo zinashuhudiwa katika miji ya Gabon kila kona kumebandikwa mabango yanayosema tupeni chochote lakini sio Ali.Na juu ya hilo mapambano ya uchaguzi huo yameingia katika mchezo wa kuchafuana ambapo hivi sasa kunasambazwa barua pepe na ujumbe wa sms unaoasema kwamba Ali Bongo ni mnigeria na sio mgabon.
Hata rubaa za kisiasa nchini humo zimekiri kwamba mambo hayakuwa shwari katika utawala wa miaka 41 wa Omar Bongo kutokana na kujilimbikizia utajiri mkubwa na pia alikuwa akichunguzwa na Ufaransa kwa madai ya rushwa.Wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini humo wanasema kwamba raia wengi wa taifa hilo wanataka mabadiliko ya uongozi nchini humo.
Mwandishi Saumu Mwasimba
Mhariri-Abdul-Rahman