Uchaguzi wa Rais leo Nigeria
20 Aprili 2007
Akitoa mwito huo, wanajeshi wa Nigeria walikamata jana lori lililopakia kura zilikwishapigwa kwa muujibu upinzani uliarifu hapo jana.
Tuhuma hizo zinafuatia ghasia na hitilafu kadhaa zilizoonekana wakati wa uchaguzi wa mikoa wiki iliopita uliokipatia chama-tawala People’s Democratic Party (PDP)- ushindi mkuu na kuvichochea vyama vya upinzani kutangaza havina imani na Tume ya Uchaguzi.
Uchaguzi wa leo utapokezana kwa mara ya kwanza madaraka kutoka kiongozi mmoja wa kiraia aliechaguliwa kumkabidhi mwengine aliechaguliwa.
Watetezi wa usoni na maarufu katika uchaguzi wa leo wa rais ni kati ya mtetezi wa chama-tawala PDP mwenye kuungwamkono na rais Obasanjo-Umaru Yar’Adua upande mmoja,makamo-rais anaesimamia chama cha Action Congress Atiku Abubakar na mtetezi wa chama cha Upinzani cha All Nigeria People’s Party Muhammadu Buhari.
Uchaguzi wa leo azma yake hasa ni kuimarisha utawala wa kiraia katika nchi yenye historia ndefu ya utawala wa kijeshi.
Nigeria ndilo dola lenye wakaazi wengi kabisa barani Afrika na uchaguzi wa leo ukitazamiwa kuonesha demokrasia inapiga hatua mbele barani humo.
Lakini,tayari upinzani umefichua kuwa wanajeshi wa Nigeria jana wamelikamata lori lililosheheni kura zilizokwishapigwa huko aduna,kaskazini mwa Nigeria na hivyo, upinzani unahofia uchaguzi wa leo tayari umeshatiwa mkono.Kura katika lori hilo zimepigwa kwa chama-tawala cha PDP.
Tuhuma hizi zinafuatia mashtaka ya wiki iliopita wakati wa chaguzi za mikoa ambapo chama-tawala PDP kilinyakua ushindi wa viti 27 kati ya viti vyote 34.Wachunguzi wa uchaguzi huo walisema matokeo katika serikali 10 za mikoa yasikubaliwe. Hii ikapelekea vyama vya upinzani kuondoa imani na Tume ya uchaguzi.
Rais Olesegun Obasanjo aliwataka wachunguzi wa uchaguzi ule kuonesha subira na kutambua kasoro ziliopo nchini Nigeria na hivyo, kutotia chumvi mabaya yaliopita.
Watetezi 2-wanaempinga Umaru Yar’Adua walidai hapo kabla kuahirishwa uchaguzi wa leo hadi kwanza Tume ya sasa ya uchaguzi imevunjwa na mpya imeteuliwa.Pia walidai matokeo ya uchaguzi wa mikoa ya wiki iliopita yafutwe.
Rais Obasanjo lakini alisema kwamba uchaguzi wa leo unasonga mbele na viongozi wa upinzani wakaamua kushiriki .
Obasanjo anatumai mtetezi asie maarufu sana wa chama-tawala Yar’Adua atawika.Upinzani imemuita ni ‘kibaraka’ na wakosoaji wadai rais Obasanjo anataka kuendelea kutawala nyuma ya pazia baada ya kulazimishwa binafsi an’gatuke aliposhindwa kubadili katiba ya Nigeria kumruhusu kugombea wadhifa wa urais kwa kipindi cha tatu.