1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchumi wa Afrika kuporomoka

9 Aprili 2020

Benki ya dunia imesema uchumi wa bara la Afrika,Kusini mwa jangwa la Sahara utaporomoka kwa kiwango ambacho hakijashuhudiwa tangu miaka 25 iliyopita,kutokana na virusi vya Corona

https://p.dw.com/p/3ah5Y
USA Weltbank-Zentrale in Washington
Picha: Reuters/Y. Gripas

Mripuko wa virusi vya Corona unaozidi kusambaa unatarajiwa kuzisukuma nchi za Afrika,Kusini mwa Jangwa la sahara katika mporomoko wa kiuchumi katika mwaka huu 2020 kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 25. Huo ni utabiri uliotolewa na benki ya dunia.

Ripoti ya benki ya dunia kuhusu hali ya kiuchumi barani Afrika imesema kwamba uchumi wa bara hilo utashuka asilimia 2.1 na kufikia asilimia 5.1 kutoka kiwango cha ukuaji cha mwaka jana cha asilimia 2.4.

Aidha mripuko huu wa virusi vya Corona utazigharimu nchi za ukanda wa kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika dola bilioni 37 hadi dolla bilioni 79 ambayo ni hasara itakayoonekana mwaka huu kufuatia kuvurugwa kwa shughuli nyingi za kibiashara na kiuchumi miongoni mwa sababu nyinginezo.

Nigeria Corona-Pandemie Polizei
Polisi wa Nigeria katika kukabiliana na janga la coronaPicha: Getty Images/AFP/P.-U. Ekpei

Hali ilivyo barani Afrika

Bara la Afrika lina alau visa 10,956 vya watu waliothibitika kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona, vifo 562 na waliopona wakiwa ni 1,149 kwa mujibu wa mahesabu yaliyofanywa na shirika la habari la Reuters kwa kuzingatia taarifa zilizokwishatolewa na serikali na data za shirika la afya duniani WHO.

Makamu mwenyekiti wa benki ya dunia kwa ajili ya Afrika Hafez Ghanem amesema janga la ugonjwa wa Covid-19 linapima uwezo wa mwisho wa jamii na nchi zote ulimwenguni na kuna uwezekano hususan kwa nchi za Afrika kuathirika zaidi.

Jitihada za utoaji wa fedha za dharura

Benki ya dunia na shirika la fedha la kimataifa IMF zinakwenda mbio kutoa fedha za dharura kwa nchi za Afrika na nyinginezo kukabiliana na virusi vya Corona ili kupunguza athari zitakazosababishwa na hatua za kufungwa kwa shughuli za kimaisha zinazochukuliwa nchi mbali mbali ulimwenguni kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo vya Corona.

Ikumbukwe kwamba janga la virusi vya Corona limesababisha kufutwa kwa safari za kimataifa katika nchi nyingi za bara hilo la Afrika hali ambayo imeathiri kwa kiwango kikubwa sana sekta mbali mbali kama vile sekta ya utalii.
Serikali mbali mbali za bara hilo la Afrika zimetangaza hatua ya kufunga miji au nchi kwa maana ya kwamba hakuna shughuli za kawaida za kimaisha haziruhusiwi tena kufanyika au baadhi ya nchi zimetangaza kuzuia watu kutoka nje,hizi zikiwa ni hatua zinazodhamiriwa kupunguza kusambaa kwa virusi vya Corona ambavyo kwa hakika vimechelewa kuingia Afrika lakini sasa vinasambaa kwa kasi kubwa barani humo kwa mujibu wa W.H.O.

Kutokana na hali hii benki ya dunia inasema  ukuaji wa pato la ndani utapungua kwa kiwango kikubwa na hasa katika nchi tatu zenye uchumi mkubwa katika bara hilo,Nigeria,Angola na Afrika Kusini. Kadhalika nchi zinazouza mafuta pia zitaathirika sana.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Josephat Charo

Source-The World Bank/ RTRE

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW