Uchumi wa Lebanon waathirika kutokana na mgogoro wa kisiasa
24 Agosti 2018Matatizo ambayo yamekuwa yakishuhudiwa nchini humo kwa miaka, na kuingia kwa idadi kubwa ya wakimbizi milioni 1.5 tangu mwaka 2011, vimechangia taifa la Lebanon kuendelea kukabiliwa na misukosuko. Nchi hiyo imeorodheshwa ya tatu duniani kwa kuwa na kiwango kikubwa cha deni ambacho ni dola bilioni 81 au asilimia 152 ya Pato la Taifa.
Kutokuwapo kwa serikali mpya kumeifanya Lebanon kushindwa kupata mabilioni ya pesa kutoka kwa wafadhili wa kimataifa ili kuwekeza katika mataifa ya nje katika miundo msingi na miradi mingine. Hayo yanajiri huku biashara nyingi zikifungwa, baadhi ya kampuni zikiwafuta kazi wafanyakazi, na hata raia wa Lebanon wanaoishi katika eneo la Ghuba ya Uajemi wakishuhudia kushuka kwa mapato katika biashara zao kutokana na kushuka kwa bei za mafuta.
Licha ya hali hiyo, raia wengi ambao wana pesa sasa wameamua kutumia pesa kidogo kwa matumizi yao wakihofia maisha yao ya baadaye yatakavyokuwa. Wakazi wanalalamika kwamba wanalazimika kulipia zaidi kwa kila kitu kukiwemo jenereta za binafsi ili kukabili tatizo la kukatiwa umeme na malori yanayowaletea maji miezi ya kiangazi.
Serikali mapema mwaka huu ilisitisha kutoa mikopo ya kudumu ya nyumba yenye kiwango kidogo cha riba kwa sababu idadi kubwa ya wanaoomba mikopo imechangia kupungua kwa fedha zilizokuwepo. Hakuna siku inayopita bila wanasiasa kuonya kuwa huenda hali ikawa mbaya zaidi, suala ambalo linazua hofu miongoni mwa raia wa Lebanon.
Tofauti za kisiasa zimechelewesha utekelezwaji wa mikopo na ruzuku zilizoahidiwa wakati wa kongamano la kiuchumi jijini Paris mwezi Aprili. Wafadhili wa kimataifa waliahidi kutoa dola bilioni 11 kwa Lebanon lakini wafadhili hao walitaka kuhakikisha fedha hizo zinatumika vizuri katika nchi hiyo inayokabiliwa na tatizo la ufisadi.
Lakini licha ya kuwepo mgogoro huo, mwaka uliopita serikali iliidhinisha kiwango cha mishara cha wafanyakazi wa umma ambayo itagharimu dola milioni 800 kila mwaka. Serikali iliweka kodi mpya kushughulikia mfumo wa mishahara, hivyo kuongeza mzigo kwa raia ambao tayari wamekuwa wakiathirika kutokana na kodi za kiwango cha juu bila kupata faida katika huduma za maji na umeme.
Gavana wa Benki Kuu nchini humo Riad Salameh amekuwa akitoa taarifa mara kwa mara kuwahakikishia wananchi wa nchi hiyo kwamba sarafu iko imara. Mwanauchumi Kamel Wazne anasema,´´Kumeshuhudiwa matatizo serikalini lakini kwa sasa pauni ya Lebanon iko salama. Benki Kuu ianajaribu kuwa na sarafu za dola katika hifadhi zake iwapo kutatokea mgogoro wa kiuchumi.´´
Lebanon yatathmini kurejelea uhusiano na Syria
Waziri Mkuu Saad Hariri, ambaye amekuwa akiyaomba mataifa ya Magharibi kuwapa msaada, ana wasiwasi kutokana maelezo ya kuundwa kwa serikali na tofauti miongoni mwa wanasiasa kufuatia iwapo Lebanon inafaa kurejelea mawasiliano na serikali ya Rais wa Syria Bashar Assad.
Hariri amekuwa akishinikizwa kurejelea mazungumzo na Syria ili kuongeza bidhaa zinazosafirishwa kutoka Lebanon kupitia mpaka wa Naseeb na Jordan, ambao ulitwaliwa na wanajeshi wa Syria kutoka kwa wapiganaji mnamo mwezi Julai. Hariri ni mkosoaji mkubwa wa Rais Assad ndio maana anapinga kurejelewa kwa uhusiano na Rais huyo.
Mwandishi: Sophia Chinyezi/APE
Mhariri: Iddi Sessanga