1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchunguzi AP: Familia za Wapalestina kuangamizwa Gaza

17 Juni 2024

Shirika la Habari la Associated Press (AP) limefanya uchunguzi kuhusu kuangamizwa kwa familia za Wapalestina katika Ukanda wa Gaza kwenye operesheni ya kijeshi ya Israel ya anga na ardhini, inayoendelea.

https://p.dw.com/p/4h9rN
Bureij, | Ukanda wa Gaza | Wapalestina wakiondoka eneo la mashambulizi yaliokithiri ya Israel.
Baadhi ya familia za Kipalestina zilizosalia zikiondoka katika eneo la Bureij baada ya kukabiliwa na mashambulizi ya Israel.Picha: Ali Jadallah/AA/picture alliance

Uchunguzi huo umebaini kwamba maangamizi hayo yamefikia kiwango ambacho hakijawahi kuonekana. 

Uchunguzi huo wa shirika la habari la AP umeelezea kwamba mashambulizi ya anga na ya ardhini yanayofanywa na jeshi la Israeli katika operesheni yake kwenye Ukanda wa Gaza yanasababisha maafa kwa sababu wakati mwingine familia nzima inaangamia hadi kufikia vizazi vinne pale familia hizo zinapokuwa zimejihifadhi mahala kwa pamoja kwa kudhania kuwa wako mahala salama ambako hawawezi kufikiwa na mashambulio ya mabomu ambayo mara nyingi hufanyika bila kutolewa taarifa ya mapema kwamba eneo husika litashambuliwa. 

Uchunguzi wa shirika la Habari la Associated Press umebaini kwamba Wapalestina wasiopungua 60 waliuawa katika milipuko ya mabomu kati ya miezi ya Oktoba na Desemba mwaka jana. Na kwamba huo ulikuwa ni wakati mbaya zaidi ambapo vita hivyo vya Israel dhidi ya kundi la Hamas vilisababisha uharibifu mkubwa. Vita hivyo sasa vimeingia katika mwezi wake wa tisa sasa.

Miongoni mwa familia zilizoathirika zaidi ni familia ya Mughrabi ambapo zaidi ya wanafamilia 70 waliuawa katika shambulizi moja la anga la Israel lililofanyika mnamo mwezi Disemba mwaka jana.

Soma pia:UN yakaribisha tangazo la Israel la kusitisha mapigano kwa muda Gaza kuruhusu misaada zaidi kupelekwa katika eneo hilo

Familia nyingine ya Abu Najas iliwapoteza wanandugu wapatao 50 waliouawa wakati mmoja kwenye mashambulizi mnamo mwezi Oktoba, na miongoni mwa waliouawa walikuwemo angalau wawili  na kina mama wajawazito.

Ukoo mwingine mkubwa ulioathiriwa ni ule wa Doghmush ambao uliwapoteza takriban wanafamilia 44 katika mashambulio yaliyoulenga msikiti mmoja ambapo wiki chache baadae idadi ya waliofariki ilipanda na kufikia watu 100.

Baadhi ya familia zimeangamizwa 

Magofu ya makaazi yakisalia tupu baada ya Israel kushambulia.
Magofu ya makaazi yakisalia tupu baada ya Israel kushambulia.Picha: Dawoud Abo Alkas/AA/picture alliance

Mambo yaliyogusiwa kwenye ripoti ya shirika la Habari la AP ni pamoja na kubainika kuwa kwenye baadhi ya familia hakuna hata mwanafamilia mmoja aliyesalia ambaye angeweza kutoa kumbukumbu juu ya matukio yaliyoikuta familia yake.

Ripoti hiyo ya uchunguzi inasema maelfu ya Wapalestina wanashindwa kutoa hesabu kamili ya wafu kutoka kwenye familia zao kutokana na kwamba bado miili mingi imefukiwa chini ya vifusi.

Taarifa hiyo pia imetumia vyanzo vya wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas katika Ukanda wa Gaza, taarifa za wanafamilia, majirani, kurasa za mitandao ya kijamii, maelezo ya mashuhuda na watu walionusurika, pamoja na data kutoka kwa shirika la Airwars, linalofuatilia migogoro lenye makao yake mjini London.

Wakati huo huo ripoti hiyo ya uchunguzi ya shirika la Habari la AP imesema zaidi ya watu 80 wa familia ya Abu al-Qumssan ni miongoni mwa watu waliouawa.

Soma pia:Jeshi la Israel lakubali kusitisha mapigano kwa muda kuruhusu misaada kuingia Kusini mwa Gaza

Hussam Abu al-Qumssan ni mmoja wa wanafamilia hiyo aliyenusurika amesema kutokana na kwamba Gaza imezingirwa ni vigumu kabisa kwa wanahabari wa nje au wachunguzi wa kujitegemea kuweza kufika katika eneo hilo.

Mahakama kuu ya Kimataifa ya Haki inatafakari iwapo Israel inatekeleza mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina huko Gaza.

Craig Jones, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Newcastle, amesema Israel imepuuza waziwazi viwango vya vifo vya raia, katika vita hivyo vilivyochochewa na hasira baada ya kundi la Hamas kuvamia ardhi ya Israel na kuwaua watu zaidi ya elfu moja na kuwateka wengine mnamo Oktoba 7.

Ramy Abdu, mwenyekiti wa shirika la Haki za Binadamula EuroMed, linalofuatilia vita vya Gaza lenye makao yake mjini Geneva, amesema Wapalestina daima watazikumbuka familia zote ambazo zimetoweka machoni na kwenye maisha yao, amesema vita vya Gaza ni kama kijiji au kitongoji kizima kimeangamizwa.

Idadi ya vifo na majeruhi yaongezeka Ukanda wa Gaza