Ufisadi wasukuma asilimia 60 ya vijana kuihama Afrika
4 Septemba 2024Kulingana na ripoti ya taasisi hiyo yenye makao yake mjini Johannesburg Afrika Kusini, ambayo ilianzisha utafiti wa kukusanya maoni miongoni mwa vijana 5,604 wenye umri kati ya miaka 18 hadi 24, Ufisadi unaonekana kama kizingiti kikubwa zaidi wanachokabiliana nacho kufikia uwezo wao wenyewe na maisha bora.
Ripoti hiyo inaendelea kusema kuwa zaidi ya yote, vijana hawaamini kuwa serikali zao zinafanya vya kutosha kukabiliana na janga hilo na kutokana na hilo karibu asilimia 60 wanatazamia kuhama katika miaka mitano ijayo.
Kwa mujibu wa utafiti wa Vijana wa Afrika wa 2024, taasisi hiyo inasema hauna kifani katika upeo na ukubwa, na ulifanyika kupitia mahojiano ya ana kwa ana kuanzia mwezi Januari na Februari nchini Botswana, Cameroon, Chad, Congo Brazzaville, Côte d'Ivoire, Ethiopia, Gabon, Ghana, Kenya, Malawi, Namibia, Nigeria, Rwanda, Afrika Kusini, Tanzania na Zambia.
Soma piaUganda yawazuilia waandamanaji kadhaa wanaopinga ufisadi:
Amerika Kaskazini ilikuwa chaguo bora kwa uhamiaji miongoni mwa kikundi cha umri uliofanyiwa mahojiano, ikifuatiwa na nchi za Ulaya Magharibi kama vile Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Uhispania.
Zaidi ya nusu ya waliohojiwa walisema Afrika inaelekea katika mwelekeo mbaya, ingawa kulikuwa na ongezeko la wastani hadi asilimia 37 la kile kilichotajwa kama "matumaini ya Afrika" ikilinganishwa na utafiti wa 2022.
Taasisi hiyo inasema vijana wanataka vikwazo vikali zaidi dhidi ya wanasiasa mafisadi, ikiwa ni pamoja na kuwapiga marufuku kugombea nyadhifa na pia wanataka aina tofauti ya serikali.
Imani katika mifumo ya utawala wa kijeshi
Karibu theluthi mbili ya waliohojiwa wanaamini demokrasia, huku karibu asilimia 60 waliunga mkono mfumo wa uongozi wa Kiafrika.
Takriban mmoja kati ya watatu wanaamini kuwa mifumo isiyo ya kidemokrasia, kutoka kwautawala wa kijeshi au wa chama kimoja, inaweza kuwa bora katika hali fulani.
Wengi wa waliohojiwa walisema ushawishi wa kigeni ni suala kuu. Wana wasiwasi na nchi zao kunyonywa na makampuni ya kigeni hasa madini yao ya asili kuchimbwa na kusafirishwa nje ya nchi bila manufaa yoyote kwa wananchi.
Soma pia: Mbio mpya za lithium zachochea ufisadi na kuzuru jamii Afrika
Takriban asilimia 82 kati yao waliona ushawishi wa China kuwa chanya, huku asilimia 79 wakisema vivyo hivyo kwa Marekani.
Mitazamo ya ushawishi wa Urusi iliongezeka, haswa nchini Malawi na Afrika Kusini, huku zaidi ya nusu ya wale wenye mtazamo chanya kuhusu Urusi wakitaja utoaji wake wa nafaka na mbolea.
Wengi walisema ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi wa rais wa Marekani utakuwa matokeo mabaya zaidi kwa Afrika kuliko ushindi wa mgombea wa chama cha Democratic Kamala Harris.
Kulingana na mkurugenzi wa mawasiliano wa taasisi hiyo Nico De Klerk, Utafiti wa Vijana wa Afrika, uliofanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2020, unalenga "kutoa sauti kwa vijana wa Afrika kwa njia ya kisayansi." Pia hutoa data muhimu kwa serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na wawekezaji.
Afrika ni nyumbani kwa karibu vijana milioni 420 wenye umri wa kati ya miaka 15-35, theluthi moja miongoni mwao hawana ajira, kwa mujibu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika. Huku Idadi ya watu ikitarajiwa kuongezeka maradufu hadi zaidi milioni 830 ifikapo 2050.