Udhalilishaji wa watoto Ujerumani watisha
7 Juni 2019Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto 136 waliuawa kinyama mwaka 2018, ambapo asilimia 70 ya waathirika walikuwa chini ya umri wa miaka 6. Watoto wengine 98 walikuwa pia wahanga wa majaribio ya mauaji.
Idadi ya watoto waliodhalilishwa kingono mwaka uliopita iliongezeka kwa asilimia 6.43 kutoka mwaka 2017, na kufikia visa 14,600 -- ambao ni wastani wa visa 40 kila siku.
Tunafikiri visa vingi haviripotiwi
Polisi inasema tarakimu halisi zinaweza kuwa juu zaidi, lakini mnamo wakati wakosaji wana kawaida ya kuwa wanafamilia, marafiki au majirani, inakuwa vigumu mara nyingi kwa watoto kuripoti uhalifu kama huo.
Rais wa Ofisi ya shirikisho inayoshughulikia uhalifu nchini Ujerumani (BKA), Holger Münch, alisema ingawa polisi waliweza kutatua karibu asilimia 80 ya kesi walizoshughulikia kuhusu udhalilishaji wa watoto kingono, takwimu zinawakilisha tu uhalifu ulioripotiwa polisi. Akaongeza kuwa "tunahisi - na watalaam wakadiria - kuwa uhalifu mwingi unapita bila kutambuliwa."
Polisi pia iligundua visa 7,449 vya utengenezaji na usambazaji wa picha za kingono za watoto katika mwaka 2018, ongezeko la asilimia 14 zaidi ya mwaka 2017. Ofisi ya BKA inasema kugundulika kwa kesi kama hizo kulitokana kwa sehemu kubwa na ushirikiano wa kimataifa.
Mwanzoni mwa mwezi Mei, maafisa wa usimamizi wa sheria nchini Marekani waliwashtua wenzao wa Ujerumani kuhusu mkururu wa picha zilizowawezesha polisi kutumia njia za kiufundi kuwabaini na kuwakamata wahalifu.
Maafisa wanasema hata hivyo, kwamba sheria za faragha za Ujerumani zinazokataza kuhifadhiwa kwa anuani mitandao zimekwamisha juhudi nyingi za kufichua uhalifu kama huo.
Münch ameomba kuwepo na kipindi cha kuhifadhi data kwa muda wa wiki 10 kuzisaidia mamlaka katika kuwasaka wahalifu. Alisema katika vidokezo 4000 kati ya 20,000 ilivyopokea BKA, anuani za intanet ndiyo zilikuwa zana pekee waliokuwa nayo.
Kuelewa bila kuchukua hatua hakuwasaidii wahanga
Johannes-Wilhelm Rörig, kamishna wa shirikisho anaeshughulikia masuala ya ukiukaji wa kingono, amesema kuelewa hisia bila kujifunga kuchukuwa hatua, hakutawasaidia wahanga wa udhalilishaji.
Badala yake, alizitolea mwito serikali za majimbo kuteuwa na kuwawezesha makamishna wao wenyewe, na kushughulikia tatizo kwa muktadha wa kulizuwia.
Pia alitoa wito wa hatua za kushughulikia upungufu wa ufadhili na mafunzo kwenye ofisi ya huduma kwa vijana ya Ujerumani.
"Undeni kamisheni za majimbo kuhusu udhalilishaji wa watoto. Kubalieni juu ya hatua imara na zinazofungamanisha kwa ajili ya kuingilia na kuzuwia," alisema.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/dw
Mhariri: Mohammed Khelef