1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udhibiti wa mipaka waanza Ulaya

6 Oktoba 2016

Shirika jipya la kudhibiti mipaka na pwani la Umoja wa Ulaya leo hii limezindua shughuli zake katika mpaka baina ya Bulgaria na Uturuki, huku Umoja huo ukitarajia hatua hiyo itamaliza mzozo miongoni mwa wanachama.

https://p.dw.com/p/2Qy4X
Bulgarien Türkei Grenze - Start von Frontex Grenz- und Küstenschutzagentur
Picha: Getty Images/AFP/D. Dilkoff

Maafisa wa Umoja wa Ulaya wamezindua mpango huo leo katika kivuko cha mpaka wa Andreevo ulioko baina ya Uturuki na Bulgaria ambao wahamijai wengi huutumia ili kuingia katika bara la Ulaya.  Lengo la kuanzishwa kwa kikosi hicho cha kudhibiti mipaka katika Umoja wa Ulaya ni kutafuta mfumo sawia utakao tumiwa kupambana na swala la uhamiaji haramu.

Waziri wa mambo ya ndani wa Bulgaria  Rumyana Bachvarova  amesema kuwa uzinduzi huo wa leo ni jambo  muhimu kwa bara zima la Ulaya kuweza kutokea. Pia ameeleza kwamba kuzinduliwa kwa shirika hilo jipya ni mwanzo wa ushirikiano mzuri na hatua zitakazoleta mafanikio katika mipaka ya Ulaya.

"Kuilinda mipaka yenye uhakika ndio jukumu letu kubwa hasa katika wakati huu wa mgogoro wa wakimbizi. Ili kufanikisha zoezi hili, tunahitaji kugawana majukumu na pia kufanya kazi kwa pamoja, sisi kama wanachama wa Umoja wa Ulaya vile vile kwa mashirika yetu. Nina uhakika kwamba kuanzia leo shirika hili jipya la kudhibiti mipaka na pwani litaboresha shughuli zinazohusiana na mipaka ya nchi kavu, angani na majini katika hatua ambazo zitaleta usalama kwa kiwango cha juu katika Umoja wa Ulaya."   

Griechenland Lesbos Rückführung von Flüchtlingen in die Türkei
Wakimbizi katika mpaka wa Uturuki na Ugiriki wakidhibitiwa na walinzi wa mpakani, Frontex.Picha: Reuters/G. Moutafis

Wakati huo huo kamishna wa Umoja wa Ulaya Dimitris Avramopoulos ameisifu hatua hiyo kuwa ni hatua mojawapo ya maendeleo katika historia ya kudhibiti mipaka barani Ulaya wakati alipozungumza na waandishi wa habari leo hii.

"Shirika la kudhibiti mipaka na pwani limekuwa sasa ni jambo la kweli hili limewezekana katika kipindi cha chini ya miezi tisa tangu Kamisheni ya Umoja wa Ulaya ilipolipendekeza.  Wananchi wa Ulaya wametaka na wana haki ya kupata majibu ambayo leo hii tumeyatoa majibu hayo kwa pamoja."
  
Kamishna huyo aliongezea kusema kuwa Shirika hilo jipya la kudhibiti mipaka na pwani la Umoja wa Ulaya limejengwa katika misingi ya ushirikiano na kugawana majukumu ya kulinda hata mipaka ya nje ya Umoja huo ni sawa na kusema mipaka ya nje ya nchi moja mwanachama  ni jukumu la nchi nyingine wanachama.

Kansela Angela Merkel amezungumzia jinsi Ujerumani inavyokemewa na nchi za Ulaya ya Kati na ya Mashariki kutokana na sera zake za mlango wazi kwa wahamiaji, sera ambazo wanadai kuwa zimewarahisishia wanaharakati wa kutoka kwenye makundi ya Kiislamu yenye misimamo mikali kuweza kuingia katika nchi za Ulaya na kufanya mashambulio ya kigaidi. Wahalifu hao huingia Ulaya kwa kusingizia kuwa ni wakimbizi.

Mwandishi: Zainab Aziz/DW English
Mhariri: Iddi Ssessanga