1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UEFA kuamua kuhusu mashindano ya msimu huu

15 Juni 2020

Kamati kuu ya Shirikisho la vyama vya kandanda Ulaya – UEFA itaamua Jumatano namna ya kukamilisha mashindano ya msimu huu ya Champions League na Europa League ambayo yamesitishwa kutokana na janga la COVID-19

https://p.dw.com/p/3dnmY
Schweiz UEFA Hauptquartier in Nyon
Picha: picture-alliance/dpa/J.-C. Bott

Fainali ya Champions League awali ilipangwa kuchezwa mjini Instabul, Uturuki na Europa League kuchezwa Gdansk, Poland, lakini UEFA ikasema mwezi uliopita kuwa kuna mapendekezo kadhaa yanayozingatiwa kwa ajili ya kukamilisha mashindano hayo mawili.

Mapendekezo ya UEFA huenda yakajumuisha kucheza hatua zilizobaki za kila shindano katika uwanja mmoja na kupunguza mechi za robo fainali na nusu fainali kwa mkondo mmoja tu badala ya miwili.

Mikondo ya pili ya mechi nne za hatua ya 16 za mwisho ya Champions League inapaswa kuchezwa, huku Atletico Madrid, Paris St Germain, Atalanta na RB Leipzig zikiwa tayari zimejikatia tiketi ya robo fainali. Katika Europa League, duru mbili za mkondo wa kwanza wa hatua ya 16 zinapaswa kuchezwa pamoja na mechi zote za mkondo wa pili.

Mkutano huo pia utajadili ratiba iliyopangwa na viwanja vya mashindano ya Euro 2020, ambayo yaliahirishwa hadi 2021, na tarehe za mechi za mchujo ambazo zilistahili kuchezwa Machi. Kinyang'anyiro hicho kitaandaliwa katika miji 12 kote Ulaya.