1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UEFA kuivua Moscow uenyeji wa fainali ya Ligi ya Mabingwa

24 Februari 2022

Shirikisho la soka barani Ulaya UEFA limeitisha mkutano wa dharura wa kujadili maamuzi ya kuhamisha fainali ya Ligi ya Mabingwa nje ya Urusi baada ya Moscow kuivamia Ukraine siku ya Alhamisi.

https://p.dw.com/p/47Xhd
Champions League - Round of 16 Draw
Picha: UEFA/Handout via REUTERS

Serikali ya Uingereza inaongoza katika mwito wa kusimamishwa mechi hiyo ambayo iliratibiwa kuchezwa katika uga wa St. Petersburg nchini Urusi mnamo Mei 28.

Mkutano huo wa dharura wa kamati kuu ya UEFA utafanyika siku ya Ijumaa ``ili kutathmini hali na kuchukua maamuzi muhimu,'' bodi hiyo inayoongoza ya soka barani Ulaya ilisema katika taarifa yake.

soma Marekani, washirika waiwekea vikwazo zaidi Urusi

Ligi Kuu ya Ukraine ilisimamisha shughuli zake siku ya Alhamisi kutokana na uamuzi wa Rais Volodymyr Zelenskyy wa kuweka sheria ya kijeshi. Ligi hiyo imekuwa kwenye mapumziko ya miezi miwili ya msimu wa baridi na ilipaswa kurejea Ijumaa.

Hata hivyo Ukraine haikutoa tarehe yoyote iliyopangwa kuanza upya.

Mzozo watatiza michezo

Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki ya Walemavu (IPC) ilisema ilikuwa kwenye mazungumzo na maafisa wa michezo nchini Ukraine na Urusi huku timu zao zikijiandaa kuelekea China kwa ajili ya kuanza kwa Michezo ya Walemavu wiki ijayo.

`IPC iko kwenye mazungumzo na Kamati za Michezo ya Walemavu ya Ukrane na Urusi kabla kuanza kwa michezo ya Majira ya baridi ya Olimpiki ya Walemavu ya Beijing 2022o,'' ilisema Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki ya Walemavu  katika taarifa iliyotumwa kwa barua pepe.

Aidha Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki ya Walemavu imedokeza kuwa kama shirika lisiloegemea upande wowote wa kisiasa, lengo lake linasalia kwenye michezo ijayo badala ya hali inayoendelea.

soma Raundi ya mtoano ya 16 bora Champions League kuanza

Tayari jina la Urusi, bendera na wimbo wa taifa zimezuiwa kutumika katika Michezo ya Olimpiki ya Walemavu huko Beijing kuanzia  Machi 4-13 juu ya mizozo ya hapo awali ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli.

Huku haya yakijiri Klabu ya soka ya Ujerumani yaiondoa kampuni ya Urusi ya Gazprom kutoka kwenye  jezi zao. Nembo ya kampuni kubwa ya nishati inayomilikiwa na serikali ya Urusi ya Gazprom imeondolewa kwenye jezi za  timu ya soka ya Schalke kufuatia uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.

 

AP