Ufaransa: Hotuba ya rais Emmanuel Macron yapingwa vikali
11 Desemba 2018Rais Emmanuel Macron katika hotuba yake alilenga miongoni mwa hatua nyingine kutuliza maandamano ya vuguvugu lijulikanalo kama vizibao vya manjano. Maandamano hayo yamefanyika mjini Paris na miji mingine ya Ufaransa kwa wiki nne mfululizo kupinga sera za kiuchumi za Rais Macron.
Hotuba ya rais wa Ufaransa imekumbana na uasi kwa kupingwa vikali na waandamanaji hao ijapokuwa wapo baadhi ya watu ambao wanazikubali juhudi za rais huyo wa Ufaransa.
Macron katika hotuba yake aliyoitoa kupitia televisheni ya taifa jana jioni aliahidi kuongeza kiwango cha kima cha chini cha mshahara kwa kiasi cha euro 100 kwa mwezi.
Katika hotuba yake ya kwanza hadharani kwa kipindi cha karibu wiki mbili, iliyochukua takriban dakika kumi na tano, Macron pia aliahidi kuwaongezea malipo watumishi wanaofanya kazi kupindukia masaa ya kazi na kuboresha maslahi ya waliosataafu lakini amekatalia mbali wito wa kurejesha sheria ya kuwatoza kodi ya juu matajiri.
Profesa Dominique Moisu mshauri maalum katika jopo la watalaamu amesema hotuba ya rais Macron ilikuwa nzuri ijapokuwa amechelewa kuitoa.
Serikali ya Ufaransa imesema unafuu wa kodi pamoja na hatua nyingine za kifedha zilizotangazwa na rais Emmanuel Macron kwa lengo la kutuliza upinzani wa nchini kote zitagharimu kati ya euro bilioni nane na 10. Hesabu hizo zimetolewa na msemaji wa serikali ya Ufaransa Benjamin Griveaux.
Msemaji huyo wa serikali ameeleza kuwa serikali ya Ufaransa itatenga fedha katika bajeti ili kuwezesha hatua hizo kutekelezwa. Harakati za kupinga sera za rais Macron zimesababisha hasara kubwa za kiuchumi kwa wafanyabiashara waliopoteza wateja. Pamoja na hatua nyingine waandamanaji waliweka vizuizi kwenye barabara.
Wanasiasa wa wanaoegemea siasa kali za mrengo wa kushoto na kulia wamepuuzilia mbali ahadi hizo za Macron wakidai kwamba hazileti mageuzi makubwa ya kiuchumi yanayohitajika. Uchunguzi wa maoni ya umma unaonesha Wafaransa wengi wanaunga mkono maandamano ya umma ya kuishinikiza serikali huku Macron umaarufu wake ukiendelea kupungua miongoni mwa Wafaransa.
mwandishi:Zainab Aziz/AFP/AP
Mhariri: Josephat Charo