1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa ina wasiwasi na hali tete ya Mashariki ya Kati

13 Mei 2018

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amemueleza Rais wa Marekani Donald Trump kuwa ana wasiwasi mkubwa kutokana na hali tete katika Mashariki ya Kati baada ya Trump kujiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya Iran.

https://p.dw.com/p/2xcP8
USA Washington - Donald Trump trifft Emmanuel Macron
Picha: Reuters/J. Ernst

Ofisi ya Rais Macron imesema kiongozi huyo wa Ufaransa jana alimpigia simu Trump na alielezea wasiwasi wake kuhusu uthabiti katika kanda ya Mashariki ya Kati.Taarifa hiyo imeeleza kuwa Macron amemueleza Trump kuwa anapinga vikali hatua yake ya kujiondoa kutoka mkataba huo kuhusu Iran uliofikiwa mwaka 2015.

Uhasama kati ya Iran na Israel umeongezeka katika siku za hivi karibuni tangu Marekani ilipojiondoa kutoka makubaliano hayo. Macron na Trump pia wamejadiliana kuhusu masuala ya kibiashara.

Serikali za Ulaya zinapambana kuokoa mabilioni ya dola katika biashara na Iran ambazo zilianza tena baada ya kusainiwa kwa mkataba huo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran. Aidha, Ufaransa na Umoja wa Ulaya zinaishinikiza Marekani kuwapa msamaha wa ushuru mpya uliowekwa katika bidhaa za chuma na aluminium zinazoingizwa nchini humo.

Zarif ziarani

Hayo yanajiri wakati ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Javad Zarif ameanza ziara ya kidiplomasia nchini China, Urusi  na Ubelgiji kujaribu kuyaokoa makubaliano hayo. Wizara ya mambo ya nje ya China na vyombo vya habari vya serikali vimeeleza kuwa Zarif anazuru leo Beijing akiwa na ujumbe mkubwa wa wanasiasa na wafanyabiashara kwa ajili ya kubadilishana mawazo na pande husika kuhusu maendeleo ya suala la nyuklia la Iran.

Pakistan Karachi - Iranischer Außenminister Mohammad Javad Zarif besucht Pakistan
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Javad Zarif Picha: Getty Images/AFP/A. Hassan

China ilihusika kwa karibu katika mazungumzo ya kufikiwa kwa makubaliano kama mmoja wa mataifa matano wanachama katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na mshirika wa kiuchumi wa muda mrefu wa Iran, huku ikinunua theluthi moja ya mafuta ya Iran.

China imeelezea kusikitshwa na uamuzi wa Trump kuiondoa nchi yake katika mkataba wa nyuklia wa Iran na imesema bado inayaunga mkono makubaliano hayo. Siku ya Jumatano, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Geng Shuang alisema kuwa nchi yake itaendeleza ushirikiano wa kawaida na wa wazi kati yake na Iran.

Ujerumani na biashara Iran

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas amesema kwamba itakuwa ni vigumu kuzilinda kampuni za biashara za Ujerumani zinazoendelea kufanya biashara nchini Iran, baada ya Marekani kuiwekea vikwazo vipya nchi hiyo. Hata hivyo, Maas amesema Ujerumani inataka kuzisaidia kampuni hizo kuendelea na biashara zake Iran.

Außenminister Heiko Maas in Litauen
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko MaasPicha: picture alliance/dpa/B. Pedersen

Maas ameliambia gazeti la Bild am Sonntag kwamba haoni suluhisho rahisi la kuzilinda kampuni kuepukana na hatari iliyopo baada ya Marekani kuweka vikwazo hivyo. Amesema nchi za Ulaya zinataka kuhakikisha kuwa Iran itaendelea kuheshimu masharti na vikwazo vilivyosainiwa katika mkataba wa nyuklia.

Ujerumani, Ufaransa pamoja na Uingereza zimesema bado zinaendelea kuyaunga mkono makubaliano ya mpango wa nyuklia wa Iran. Mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa hayo matatu yenye nguvu barani Ulaya watakutana na mwenzao wa Iran siku ya Jumanne mjini Brussels ili kujadiliana kile kitakachofuata.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, Reuters, DW https://bit.ly/2IBy5Vy
Mhariri: Caro Robi