Ufaransa kuondoa dharura kwenye kisiwa cha New Caledonia
27 Mei 2024Kulingana na vyombo vya habari nchini Ufaransa, hatua hiyo iliyochukuliwa Mei 15 kufuatia machafuko kuzuka katika eneo hilo, haitorefushwa tena na sasa itafikia mwisho kesho Jumanne.
Serikali ya Ufaransa inatarajia kwamba hatua hiyo itachochea kufanyika kwa mazungumzo. Ufaransa pia imetangaza kupeleka polisi wa ziada 480 na kufikisha idadi ya maafisa wa ulinzi wa Ufaransa huko New Caledonia kufikia 3,500.
Ingawa kuna utulivu kwa kiasi kikubwa sasa, uwanja wa ndege katika Mji Mkuu Noumea ambao ulifungwa tangu Mei 14, utaendelea kufungwa na hakuna ndege zitakazoruka hadi angalau Juni 2.
Maandamano yaliyofanywa na makundi ya wadai uhuru kwenye kisiwa hicho kilicho chini ya milki ya Ufaransa yalichochewa na mapendekezo ya mabadiliko ya katiba yaliyopangwa kufanywa na serikali mjini Paris.