1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa:Watu zaidi ya 100,000 waambukizwa virusi vya corona

Zainab Aziz Mhariri:Tatu Karema
26 Desemba 2021

Kwa mara ya kwanza nchini Ufaransa idadi ya watu 104,611 waliambukizwa virusi vya corona katika muda wasaa 24 zilizopita. Idadi hiyo haijawahi kufikiwa nchini humo tangu kuanza janga la corona.

https://p.dw.com/p/44pkq
Frankreich Coronavirus Medizinisches Personal
Picha: Daniel Cole/AP/dpa/picture alliance

Mamlaka ya afya ya Ufaransa imesema idadi ya wagonjwa wanaougua COVID-19 waliolazwa kwenye vitengo vya kuwahudumia watu wanaohitaji uangalizi mkubwa imepanda kwa wagonjwa 28 zaidi na kufikia jumla ya watu 3,282 waliolazwa kwenye vyumba hivyo vya watu mahututi.

Serikali ya Ufaransa itafanya mkutano kwa njia ya video hapo kesho Jumatatu ambapo Rais Emmanuel Macron pamoja na wakuu mabalimbali katika utawala wake watajadili hatua mpya za kujikinga na athari zinazosababishwa na janga la corona huku wasiwasi ukiwa unaoongezeka juu ya virusi vya aina ya Omicron vinavyoenea kwa haraka.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron Picha: Julien Mattia/Le Pictorium/MAXPPP/dpa/picture alliance

Kwingineko barani Ulaya polisi wa Ujerumani walilifunga tamasha katika jiji la kaskazini la Hamburg lililohudhuriwa na watu wapatao 800 ambao kwa mujibu wa polisi hawakuwa wakizingatia sheria zinazokataza watu kukusanyika.

Kulikuwa na matukio wakati wa operesheni hiyo ya polisi ikiwa ni pamoja na ukumbi kuharibiwa baada ya polisi kuwaamuru waandaaji wa tamasha hilo kulisimamisha.

Huku aina mpya ya kirusi cha omicron sasa ikiwa imeenea katika majimbo yote ya Ujerumani, vikwazo vipya vinatarajiwa kutangazwa baada ya kumalizika sherehe za sikukuu za Krismasi na mwaka mpya.

Waqziri wa afya wa Ujerumani Karl Lauterbach
Waqziri wa afya wa Ujerumani Karl LauterbachPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture-alliance

Taasisi inayosimamia maradhi ya kuambukiza nchini Ujerumani, Robert Koch (RKI) ilimeorodhesha maambukizi mapya 22,214 ya corona katika wakati huu wa Krismasi. RKI imesema mpaka sasa idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona nchini Ujerumani imefikia karibu watu milioni 7. RKI pia imeorodhesha vifo vipya 157 vya watu waliokufa kutokana na ugonjwa wa COVID-19.

Nchini Uingereza maelfu ya watu waliiutumia wakati wa sherehe za Sikukuu ya Krismasi kupata chanjo za nyongeza katika maeneo mbalimbali kote nchini humo. Maduka ya dawa yalijiunga pamoja na vituo vya kutoa chanjo vya umma katika kutoa huduma ya chanjo iliyopewa jina la "jingle jabs"  kwa lengo la kupunguza kasi ya kuenea kwa virusi vya omicron kote nchini Uingereza.

Afrika

Barani Afrika serikali ya Kenya imetangaza kuwa itatoa chanjo za nyongeza za COVID-19 kwa wakaazi ambao walishapata chanjo kamili miezi sita iliyopita. Wizara ya afya imetoa taarifa hiyo siku moja baada ya nchi hiyo kuorodhesha idadi kubwa zaidi ya watu walioambukizwa virusi vya corona kuwahi kutokea nchini humo.

Mnamo siku ya Ijumaa ilidhihirika kuwa karibu thuluthi moja ya watu waliambukizwa virusi vipya aina ya omicron katika taifa hilo la Afrika Mashariki ambalo asilimia 14 ya watu wazima wamekwisha chanjwa.

Asia

China mnamo siku ya Jumamosi ilishuhudia idadi kubwa zaidi ya watu wake walioambukizwa virusi vya corona katika muda miezi minne. Wengi wa watu walioambukizwa ni wakazi wa mji wa kaskazini-magharibi wa Xi'an.

Rais wa China Xi Jinping
Rais wa China Xi JinpingPicha: Ju Peng/Xinhua via AP/picture alliance

Huku taifa hilo la Mashariki ya Mbali lenye nguvu linapojipanga kuandaa michezo ya olimpiki ya majira ya baridi katika mji wake mkuu Beijing mnamo mwezi wa Februari mwaka ujao, viongozi wa China mnamo Alhamisi iliyopita waliweka vizuizi vikali kwa watu milioni 13 wa Xi'an.

Marekani

Na huko nchini Marekani safari za kimataifa za ndege zipatazo 4,500 zilifutwa wikendi hii ya Krismasi. Mashirika ya ndege ya United na Delta yote yameelezea sababu za hali hiyo ikiwa ni kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wafanyikazi walioambukizwa COVID-19.

Chanzo:/ https://p.dw.com/p/44pAJ